Iran yakadhibisha madai kwamba inatishia usalama wa Uingereza
Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini London umepinga vikali madai ya mkuu wa Shirika la Ujasusi la Ndani la Uingereza (MI5) kwamba Tehran inataka kutishia usalama wa Uingereza, na kuyataja madai hayo kuwa "yasiyo na msingi."
Ubalozi wa Iran mjini London, Uingereza umetoa taarifa na kukanusha madai yaliyotolewa na Sir Ken McCallum juzi ambapo ameituhumu Iran kuwa inahusika katika kile kilichotajwa kama "njama za kutekeleza mauaji na hatua za kiuhasama za kuvuka mpaka.
"Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umetoa taarifa iliyoleeza kuwa unakadhibisha vikali na moja kwa moja taarifa hizi zisizo na msingi na wala mashiko.
"Taarifa zisizo na msingi kama hizi ni sehemu ya juhudi endelevu zenye lengo la kupotosha sera za Iran na kudhoofisha uhusiano wa kidiplomasia wa pande mbili," imeongeza taarifa ya ubalozi wa Iran mjini London, Uingereza.
Ubalozi wa Iran nchini Uingereza umetoa taarifa hii baada ya Mkuu wa Shirika la MI5 kudai kuwa askari usalama wa Uingereza walizuia operesheni 20 zilizohusishwa na Iran katika ardhi ya Uingereza mwaka uliopita; madai ambayo Tehran imeyakadhibisha na kuyataja kuwa ni sehemu ya kampeni inayoendelea ya upotoshaji.