Mkuu wa majeshi ya Yemen auawa katika mashambulizi ya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/daily_news-i132084-mkuu_wa_majeshi_ya_yemen_auawa_katika_mashambulizi_ya_israel
Mkuu wa Majeshi ya Yemen, Meja Jenerali Mohammad Abd al-Karim al-Ghamari ameripotiwa kuuawa shahidi katika mashambulizi ya anga ya Israel, pamoja wapamba wake kadhaa na mtoto wake wa kiume aliyekuwa na umri wa miaka 13, Hussein al-Ghamari.
(last modified 2025-10-17T14:15:56+00:00 )
Oct 17, 2025 06:56 UTC
  • Mkuu wa majeshi ya Yemen auawa katika mashambulizi ya Israel

Mkuu wa Majeshi ya Yemen, Meja Jenerali Mohammad Abd al-Karim al-Ghamari ameripotiwa kuuawa shahidi katika mashambulizi ya anga ya Israel, pamoja wapamba wake kadhaa na mtoto wake wa kiume aliyekuwa na umri wa miaka 13, Hussein al-Ghamari.

Jeshi la Yemen limesema katika taarifa yake kwa njia ya televisheni kwamba, Jenerali al-Ghamari aliuawa shahidi alipokuwa akitekeleza majukumu yake ya kuiunga mkono na kuihami Palestina. Taarifa hiyo imemtaja yeye na wandani wake kuwa ni mujahidina thabiti waliojitolea kwa ajili ya kazi yao kwa ujuzi na uzoefu wa hali ya juu.

Licha ya pigo hilo, Jeshi la Yemen limesisitiza kuwa operesheni zake za kijeshi zitaendelea bila kusitishwa. "Msururu wa mashambulizi ya maroketi na ndege zisizo na rubani haujalegalega, na vikosi vyetu vya kijeshi vinaendelea kufanya kazi kikamilifu," imesema taarifa hiyo.

Imeongeza kuwa mashambulizi dhidi ya "adui mtenda jinai" yameongezeka na kuonya kuwa, adui Mzayuni atakabiliwa na hasara na vipigo kutokana na vitendo vyake.

Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen limemteua Meja Jenerali Youssef Hassan al-Madani kuwa Mkuu mpya wa Majeshi ya Yemen akimrithi marehemu Jenerali Mohammad Abdulkarim al-Ghomari aliyeuawa shahidi katika uvamizi wa kijeshi wa Israel.

Wakati huo huo, Kiongozi wa Ansarullah ya Yemen ameipongeza Iran kwa uungaji mkono wake usioyumba na kujitolea muhanga katika kutetea kadhia ya Palestina.

Abdul-Malik al-Houthi

Katika hotuba ya televisheni jana Alkhamisi, Abdul-Malik al-Houthi alisema kwamba Iran iliwatoa mhanga makamanda wake, akiwemo Luteni Jenerali Qassem Soleimani," katika njia ya kuunga mkono kadhia ya Palestina.

Jenerali Soleimani, shujaa wa kimataifa na shakhsia muhimu katika Mhimili wa Muqawama, aliuawa shahidi mnamo Januari 3, 2020 huko Baghdad katika shambulio la ndege isiyo na rubani iliyoidhinishwa na Rais wa Marekani, Donald Trump katika muhula wake wa kwanza wa uongozi.