Israel yashadidisha mateso kwa Wapalestina inaowashikilia kwenye magereza yake
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i136742-israel_yashadidisha_mateso_kwa_wapalestina_inaowashikilia_kwenye_magereza_yake
Jumuiya ya Wafungwa wa Palestina imetangaza kuwa, kwa mujibu wa ziara za ukaguzi zilizofanywa na wanasheria wake na ushuhuda uliorekodiwa, utawala wa kizayuni wa Israel umeshadidisha udhalilishaji na ushinikizaji wa kimfumo dhidi ya wafungwa Wapalestina unaowashikilia katika magereza yake ya kuogofya.
(last modified 2026-02-18T03:16:25+00:00 )
Feb 18, 2026 03:03 UTC
  • Israel yashadidisha mateso kwa Wapalestina inaowashikilia kwenye magereza yake

Jumuiya ya Wafungwa wa Palestina imetangaza kuwa, kwa mujibu wa ziara za ukaguzi zilizofanywa na wanasheria wake na ushuhuda uliorekodiwa, utawala wa kizayuni wa Israel umeshadidisha udhalilishaji na ushinikizaji wa kimfumo dhidi ya wafungwa Wapalestina unaowashikilia katika magereza yake ya kuogofya.

Kwa mujibu wa jumuiya hiyo, uvamizi wa mara kwa mara na uchukuaji hatua za kuwaadhibu wafungwa Wapalestina ungali unaendelea.

Kwa mujibu wa ripoti, mamia ya ushuhuda yamerekodiwa na taasisi za kitaalamu, yakithibitisha kutusiwa, kupigwa na kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji Wapalestina, wakati zinapofanywa operesheni za ukandamizaji ndani ya magereza ya utawala wa kizayuni. Baadhi ya ushuhuda huo unaonyesha kwamba wafungwa wanalazimishwa kufudikiza vichwa na nyuso zao juu ya sakafu kwa muda mrefu; hatua inayochukuliwa kwa lengo la kuwadhalilisha na kuwashinikiza kimwili.

Ripoti hizo zimetaja pia utumiwaji wa mbwa wa polisi na mabomu ya sauti wakati wa kuvamiwa magereza, ambayo, kulingana na mashahidi, hutumika kusababisha hofu na vitisho kwa wafungwa.

Jumuiya ya Wafungwa Wapalestina imeashiria pia maelezo yaliyotolewa kuhusu uvamizi kwenye magereza uliofanywa na Itamar Ben-Giver, waziri wa usalama wa Ndani wa utawala wa kizayuni kutangaza kwamba katika baadhi ya jela alizoingia mzayuni huyo mwenye misimamo ya chuki aliwadhalilisha wafungwa wa Kipalestina.

Asasi hiyo imesisitiza kwamba, video zilizosambazwa kwenye vyombo vya habari zinaonyesha sehemu ndogo tu ya yale yanayojiri ndani ya magereza ya Israel na kwamba kiwango halisi cha uhalifu wanaofanyiwa Wapalestina ni kikubwa mno.../