Ripoti: Ufaransa inakiuka pakubwa haki za watoto wahamiaji
Shirika moja la Umoja wa Mataifa limesema Ufaransa "imekiuka pakubwa na kwa utaratibu" haki za watoto wahamiaji, na kuwaacha wengi wao wakinyimwa huduma za afya na kukosa makazi.
Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Mtoto imesema katika ripoti yake kwamba, Ufaransa imekiuka pakubwa haki za watoto wahamiaji katika nchi hiyo ya bara Ulaya.
Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Mtoto imesema kuwa, tathmini zisizo sahihi za umri wa watoto wahamiaji nchini Ufaransa zimesababisha watoto wengi wahamiaji kuchukuliwa kuwa watu wazima. Ripoti hiyo inaeleza kuwa, hali hii imewafanya watoto kuwa katika hatari ya "hatari ya magendo, unyonyaji, unyanyasaji na miamala mibaya."
Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Mtoto iliongeza kuwa hakuna takwimu rasmi za watoto wahamiaji waliopatikana katika hali hii, lakini ni tatizo "lililoenea na linaloendelea".
Ripoti hiyo inaeleza kuwa Ufaransa imekiuka pakubwa wajibu wake chini ya Mkataba wa Haki za Mtoto, ikiwa ni pamoja na haki ya kupata huduma za afya, elimu, marufuku ya kuwekwa kizuizini kwa misingi ya uhamiaji, na kutendewa vitendo vya kinyama na kudhalilisha.
Habari za ukiukwaji wa haki za watoto wahamiaji nchini Ufaransa bila kujua zinaelekeza akili upande mwingine wa historia. Wakati fulani kati ya 1962 na 1984. Katika miaka hii, watoto na vijana 1,500 "walihamishwa" kutoka kisiwa cha Reunion kilicho kusini magharibi mwa Bahari ya Hindi hadi Ufaransa.