Serikali ya Tanzania yatakiwa itoe taarifa kuhusu aliko Polepole
Wanaharakati na mawakili nchini Tanzania wametoa wito kwa mamlaka za usalama nchini humo kutumia rasilimali zote kuhakikisha hali ya usalama wa Balozi mstaafu Humphrey Polepole inafahamika na kuwekwa wazi kwa umma, kufuatia taarifa zinazosambaa zikidai kuwa mwanasiasa huyo ametekwa.
Kupitia taarifa ya mawakili wa Polepole iliyotolewa jana Oktoba 6, wakili maarufu wa Tanzania, Peter Kibatala, amesema mteja wao ni mtumishi wa muda mrefu wa taifa, aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, hivyo ni muhimu mamlaka kutoa taarifa rasmi kwa umma wa Watanzania na jamii ya kimataifa kuhusu hali yake.
“Tunazitaka mamlaka za usalama wa raia na mali zao kutumia mbinu na rasilimali zote za umma kuhakikisha, na kisha kutoa taarifa kwa Watanzania na dunia kwa ujumla juu ya hali ya usalama na maslahi ya kisheria ya Balozi (mstaafu) Humphrey Polepole,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, Kibatala amesema ofisi yake itaendelea kutoa taarifa zaidi kuhusu hatua wanazochukua kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali duniani, kuhakikisha suala hilo linapata majibu ya wazi.
Tamko hilo limekuja muda mfupi baada ya Jeshi la Polisi kutangaza kuwa linaendelea kufuatilia taarifa zinazosambaa mitandaoni kuhusu madai ya kutekwa kwa Polepole, likisema kuwa bado linamsubiri aripoti katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa mahojiano.
Kwa mujibu wa polisi, Polepole alitumiwa barua ya wito kisheria ili kufika kuhojiwa kuhusu tuhuma alizozitoa mtandaoni, lakini hadi sasa hajatekeleza agizo hilo.
Hadi kufikia sasa, hakukuwa na taarifa rasmi kuhusu alipo au hali ya kiafya ya Polepole, huku mjadala kuhusu usalama wake ukiendelea kushika kasi kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.