Araqchi: Iran haiogopi kutumwa wanajeshi wa upande mwingine katika kanda hii
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i136398-araqchi_iran_haiogopi_kutumwa_wanajeshi_wa_upande_mwingine_katika_kanda_hii
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu haiogopi vitisho vya kijeshi, akisema: "Iran ni nchi nchi inayofuata diplomasia na mantiki, na wakati huo huo iko tayari kujilinda ili upande wowote usithubutu kulazimisha vita dhidi ya taifa la Iran."
(last modified 2026-02-15T09:07:51+00:00 )
Feb 08, 2026 09:10 UTC
  • Sayyid Abbas Araqchi
    Sayyid Abbas Araqchi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu haiogopi vitisho vya kijeshi, akisema: "Iran ni nchi nchi inayofuata diplomasia na mantiki, na wakati huo huo iko tayari kujilinda ili upande wowote usithubutu kulazimisha vita dhidi ya taifa la Iran."

Sayyid Abbas Araqchi, ambaye mapema leo Jumapili alikuwa akizungumza katika "Kongamano la Kitaifa la Sera za Kigeni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran", ameongeza kuwa: "Leo, kutumwa majeshi ya upande mwingine katika eneo la Magharibi mwa Asia hakututii hofu, kwa sababu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ingawa inafuata diplomasia, ina uwezo unaohitajika wa kujilinda na kuzuia mashambulizi."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kwamba sera ya kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu imejikita katika moyo wa kupigania kujitawala wa watu wa Iran na kuongeza: "Kauli mbiu kuu ya Mapinduzi ya Kiislamu ya "Kujitawala, Uhuru, Jamhuri ya Kiislamu," ilikuwa matokeo ya uzoefu mchungu wa kihistoria wa uingiliaji kati wa kigeni na ukosefu wa uhuru wa kweli katika vipindi vya kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu; uzoefu uliokuwa motisha ya watu wa Iran kudai uhuru wa kweli."

Akizungumzia kanuni za Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Abbas Araqchi amesema: "Kupinga kutishwa matakwa na kuzuia ushawishi wa kigeni ni nguzo za msingi za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, na bila kuelewa kanuni hii, sera ya kigeni ya Iran katika kipindi cha miaka 47 iliyopita haitaeleweka."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameutaja mpango wa nyuklia wa amani wa Iran kama mfano wa mbinu hiyo inayolenga kujitawala na akasema: "Msisitizo wa Iran wa kuendeleza urutubishaji wa madini ya urani si tu kwamba umejengeka juu ya haja ya kukidhi mahitaji ya kiufundi na kimaendeleo ya nchi, lakini pia unatokana na kanuni ya kutokubali amri na utawala wa kigeni; hakuna nchi yenye haki ya kuiambia Iran inachopaswa kuwa au kutokuwa nacho."

Araqchi amesisitiza kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nchi ya diplomasia na wakati huo huo imejiandaa kiulinzi; ikiwa lugha ya heshima itazungumzwa, jibu la heshima litatolewa, na kama watachagua lugha ya nguvu, Iran itajibu ipasavyo."