Uwezo wa kiuchumi wa Iran wa kushiriki katika masoko yanayoinukia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i136406-uwezo_wa_kiuchumi_wa_iran_wa_kushiriki_katika_masoko_yanayoinukia
Waziri wa Masuala ya Uchumi na Fedha wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewasili Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia, kwa ajili ya kushiriki katika mkutano wa pili wa masoko yanayoinukia.
(last modified 2026-02-08T09:23:26+00:00 )
Feb 08, 2026 09:23 UTC
  • Uwezo wa kiuchumi wa Iran wa kushiriki katika masoko yanayoinukia

Waziri wa Masuala ya Uchumi na Fedha wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewasili Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia, kwa ajili ya kushiriki katika mkutano wa pili wa masoko yanayoinukia.

Seyed Ali Madanizadeh, Waziri wa Masuala ya Uchumi na Fedha wa Iran aliwasili Riyadh, Jumamosi, tarehe 7 Februari akiongoza ujumbe wa Iran kwa lengo la kushiriki katika mkutano wa pili wa masoko yanayoinukia na kufanya mikutano ya pande mbili na wajumbe wa nchi nyingine zinazoshiriki katika kikao hicho.

Kikao hicho kinachoandaliwa kwa pamoja na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF na serikali ya Saudi Arabia, kikiwakilisha wajumbe wa zaidi ya nchi 50, kinafanyika katika mji wa Al-Ula.

Uwepo wa Waziri wa Masuala ya Uchumi na Fedha wa Iran katika mkutano huo nchini ni ishara ya diplomasia ya uchumi ya Iran kuimarika zaidi na kuwa na nafasi zaidi katika nyanja za kiuchumi kimataifa. Uwepo huu unafanyika katika hali ambayo ulimwengu unaelekea kwenye mifumo mipya ya ushirikiano kati ya nchi huru na zinazoendelea.

Iran imepata maendeleo makubwa katika nyanja za kisayansi na kiuchumi kwa kuwa na zaidi ya makampuni 7,000 amilifu yanayotegemea maarifa katika nyanja kama vile nanoteknolojia, teknolojia ya viumbe, akili mnemba na nishati mpya.

Uzalishaji mkubwa katika sekta kama vile dawa za kibayoteknolojia, dawa za redioactive, bidhaa za matibabu na viwanda vya hali ya juu vya ulinzi nchini Iran unaonyesha miundombinu muhimu ya kiteknolojia ya ndani, ambayo pia ina uwezo wa kuzalisha bidhaa zinazouzwa katika masoko ya kieneo na kimataifa.

Vyuo vikuu vya Iran na vituo vya utafiti pia vinatoa mafunzo kwa maelfu ya wataalamu katika nyanja za kiufundi na uhandisi kila mwaka, ambapo hulea na kuandaa rasilimali-watu muhimu ya uchumi unaotegemea maarifa.

Kuwa na moja ya akiba kubwa za gesi asilia na hifadhi ya nne ya mafuta duniani kumeifanya Iran kuwa moja ya nchi muhimu katika usalama wa nishati duniani. Eneo la kijiografia la Iran katika kuunganisha maeneo ya Mashariki na Magharibi mwa dunia pia kunatoa uwezekano wa kugeuzwa nchi hii kuwa kitovu muhimu cha usafiri na biashara ya kimataifa.

Nchi wanachama wa BRICS, soko linaloinukia

Iran ina soko la ndani lenye watu wapatao milioni 90 na sehemu kubwa ya rasilimali watu waliosoma na waliobobea katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kisayansi na kiteknolojia, jambo ambalo limeiweka nchi hii katika nafasi ya kipekee katika eneo hili. Viwanda vya magari, petrokemikali na chuma vya Iran ni miongoni mwa wazalishaji 10 wakubwa barani Asia katika sekta nyingi.

Ulimwengu wa leo unashuhudia kudhihiri kwa uchumi wa pande nyingi. Utegemezi mkongwe wa nchi zinazoendelea kwa nchi za Magharibi, hasa kwa Marekani, umesababisha ukosefu wa usawa katika upatikanaji wa rasilimali za kifedha na kiteknolojia, na kwa hivyo kikao cha masoko yanayoinukia huko Saudia inaweza kuwa hatua ya kubadilisha mlingano huu usio wa kiadilifu.

Mataifa huru yanaweza kuunda soko lenye ustawi wa kiuchumi kwa kuanzisha mifumo mbadala ya kifedha, kuhamisha teknolojia, uwekezaji wa pamoja katika miradi ya miundombinu na nishati safi, kuendeleza soko la pamoja la wateja kati ya nchi za Asia, Afrika na Amerika Kusini, bila kutegemea Marekani na nchi nyingine za Magharibi. Katika mfumo huu, Iran inaweza kuwa na nafasi muhimu katika uundaji wa soko hili, ikiwa kama kiungo kati ya Mashariki na Magharibi mwa Asia.

Kwa miundombinu yake ya kiteknolojia, maliasili tajiri na rasilimali watu waliobobea, Iran ina uwezo wa kuwa na nafasi muhimu katika mchakato mzima wa kuunda masoko yanayoinukia. Kushiriki kikamilifu katika mikutano hiyo sio tu kunatoa fursa ya kuanzishwa uwezo wa ndani, bali pia kunaandaa msingi wa maingiliano mazuri kati ya nchi huru na kupunguza utegemezi wa nchi hizo kwa mifumo ya kifedha na kiteknolojia ya Magharibi.

Ikitegemea uchumi uliosimama kwenye msingi wa maarifa, nishati, usafiri na ushirikiano wa kikanda, Iran inaweza kufafanua upya msimamo wake katika mpangilio mpya wa uchumi wa dunia na hivyo kuwa mojawapo ya mihimili muhimu katika mtandao uliounganishwa wa nchi zinazoendelea.

Ushiriki wa Iran wenye malengo maalumu katika kikao cha masoko yanayoinukia bila shaka ni fursa ya kunufaika na uchumi wa pande kadhaa, kuongeza mauzo ya nje yasiyo ya mafuta, kuvutia uwekezaji wa kigeni na kuimarisha uhuru wa kiuchumi.