Waziri wa Habari wa Somalia: Hatutaruhusu Israel kutumia ardhi yetu kuwatishia majirani
-
Daud Aweys Jama
Waziri wa Habari, Utamaduni na Utalii wa Somalia, Daud Aweys Jama, amesema kwamba nchi yake imethibitisha mara kwa mara msimamo wake wa kupinga na kulaani ukiukaji wa wazi wa Israel wa mamlaka ya kujitawala Somalia na ardhi yake yote.
Akizungumza kando ya Jukwaa la 17 la Al Jazeera huko Doha, Daud Aweys Jama amesema kwamba ukiukwaji huo wa sheria unaofanywa na Israel unakuja katika wakati mgumu sana kwa Somalia, kwani inashiriki katika kupambana na ugaidi wa kimataifa ndani ya ardhi yake, katika kujilinda na kama mchango kwa usalama wa kanda hiyo na Pembe ya Afrika.
Jama ameeleza kwamba ukiukaji huu wa sheria sio tu kwamba unadhoofisha usalama wa Somalia, bali unaathiri pia usalama wa eneo hilo, Pembe ya Afrika, Mashariki ya Kati na Bahari Nyekundu.
Waziri wa Habari wa Somalia ameelezea matumaini yake kwamba jamii ya kimataifa na pande zote husika zitaelewa suala la Somalia, akibainisha kuwa chaguo ambalo nchi yake imechukua ni kutumia "njia za kidiplomasia," ambazo amesema zinafanya kazi vyema kwa Somalia hadi sasa.
Akizungumzia athari mbaya za hatua na nia za Israel nchini mwake, Jama amesema kwamba jambo hilo linahatarisha usalama wa Somalia, haswa usalama wa raia wanaoishi katika eneo la Somaliland kaskazini mwa nchi. Ameeleza kwamba ajenda ya Israel ni kuanzisha kambi ya kijeshi katika eneo hilo kwa lengo la kupigana vita dhidi ya nchi au mashirika mengine, "jambo ambalo halitumikii maslahi ya Somalia au eneo hilo."
Ameashiria ripoti kwamba Waisraeli walitaka kuwahamishia Wapalestina katika eneo la Somaliland, akisema suala hili ni ukiukaji wa haki za watu wa Palestina, na kwamba jambo hili linatoa changamoto kwa amani na ya eneo hilo na usalama wa dunia kwa ujumla.