Sera ya vikwazo yakwama, Marekani yasitisha vikwazo vipya dhidi ya Iran
(last modified Mon, 02 Jun 2025 11:05:51 GMT )
Jun 02, 2025 11:05 UTC
  • Sera ya vikwazo yakwama, Marekani yasitisha vikwazo vipya dhidi ya Iran

Serikali ya Marekani imesitisha hatua za kuanzisha vikwazo vipya dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, jambo linaloashiria kufeli licha ya kampeni ya vikwazo ya mashinikizo ya juu kabisa ambayo imekuwa ikiendeshwa kwa muda mrefu dhidi ya Iran.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa Jumapili na gazeti la The Wall Street Journal, Msemaji Mkuu wa Ikulu ya White House, Karoline Leavitt, ametoa agizo kwa taasisi za serikali kusitisha mara moja shughuli zote za kuandaa vikwazo vipya dhidi ya Iran.

Agizo hilo linaripotiwa kufikishwa kwa maafisa waandamizi katika Baraza la Usalama wa Taifa (NSC), Wizara ya Fedha, na Wizara ya Mambo ya Nje. Hata hivyo, kitendo cha agizo hilo kutolewa moja kwa moja na msemaji wa Ikulu badala ya vyombo husika kama NSC au Wizara ya Fedha kimezua maswali miongoni mwa maafisa wa serikali.

Taarifa hiyo imeibua mjadala mpya kuhusu hatima ya sera ya “mashinikizo ya juu kabisa” iliyobuniwa na Rais Donald Trump wa Marekani, katika kipindi chake cha kwanza, ambayo imekuwa nguzo kuu ya sera za Washington dhidi ya Tehran.

Ingawa mpango huo ulianzishwa na Trump katika awamu yake ya kwanza, ulirithiwa na Rais Joe Biden aliyeufuatilia kwa karibu na kuuendeleza, kabla ya Trump kuurudisha kwa nguvu zaidi aliporejea madarakani.

Katika kutekeleza sera hiyo, Marekani ilijiondoa kwenye makubaliano ya kihistoria ya nyuklia ya mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani.

Katika awamu yake ya sasa, Trump ameendelea kuitisha Iran ipunguze kiwango cha kurutubisha madini ya urani hadi “sifuri,” na hata kutishia kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran. Pia amekuwa akisisitiza kurejesha kwa nguvu zaidi kampeni ya 'mashinikizo ya juu kabisa' dhidi ya Iran

Ripoti hiyo ya The Wall Street Journal imenukuu chanzo kilicho karibu na Ikulu ya White House kikisema kuwa kampeni hiyo, ambayo awali ililenga kuidhoofisha kiuchumi Iran, lakini bila mafanikio, kwa sasa imekwama kabisa.

Tangu Mei 21, hakuna tangazo lolote jipya la vikwazo lililotolewa.

Hali hiyo imezua maoni tofauti miongoni mwa maafisa wa Marekani. Baadhi wanaamini ni hatua ya muda inayolenga kupitia kwa makini vikwazo vipya kwa kuzingatia unyeti wa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yanayoendelea baina ya Iran na Marekani. Wengine, hata hivyo, wameeleza hofu kuwa maamuzi muhimu ya sera hayaeleweki na baadhi ya wahusika wameachwa nje ya mchakato.

Pia, kuna mkanganyiko kuhusu iwapo kusitishwa huku kunahusu tu vikwazo vipya au pia utekelezaji wa vile vya zamani.

Licha ya mikakati hiyo ya Marekani, Iran imesisitiza kuwa itaendelea na shughuli zake za nyuklia kwa ajili ya matumizi ya amani, bila kuyumbishwa na shinikizo la nje.