Jeshi la Israel lapata kipigo kingine kikubwa kutoka kwa HAMAS
(last modified Tue, 03 Jun 2025 07:04:44 GMT )
Jun 03, 2025 07:04 UTC
  • Jeshi la Israel lapata kipigo kingine kikubwa kutoka kwa HAMAS

Wanajeshi vamizi wa Israel wameingia kwenye mtego uliotegwa na Brigedi za Izzuddin al Qassam, Tawi la Kijeshi la HAMAS huko Jabalia, kaskazini mwa Ghaza na wamepoteza wanajeshi kadhaa.

Vyombo vya habari vya lugha ya Kiebrania vimetangaza habari hiyo huku vikitoa taarifa zinazokinzana kuhusu idadi ya wanajeshi wa Israel walioangamizwa hivi karibuni huko Jabalia, kaskazini mwa Ghaza.

Baadhi ya vyombo vya habari vya Kiebrania vimetangaza kwamba wanajeshi wengi, wasiopungua 20 waliingia kwenye mtego uliotegwa na wanamapambano wa HAMAS huko Jabalia, na wote wameuawa na kujeruhiwa. Ingawa, Kurugenzi ya Ufuatiliaji wa Habari za Kijeshi ya Israel hairuhusu kuchapishwa habari za kina kuhusiana na vipigo wanavyopata wanajeshi wa Israel huko Ghaza, lakini hata hizo habari chache zinazopitia mchujo mkali wa kijeshi, zinaonesha kuwa wanajeshi wa Israel wanaendelea kupata vipigo huko Ghaza licha ya kudai kuwa wamedhibiti kila kitu.

Mwandishi wa habari wa Israel, Daniel Amiram ameandika kwenye ukurasa wake binafsi wa mtandao mmoja wa kijamii kwamba wapiganaji wa Palestina walifyatua roketi la Yassin 105 kwenye jengo ambalo wanajeshi wa Israel walikuwa wamejichimbia na kuua na kujeruhi baadhi yao, na mara baada ya helikopta ya kijeshi ya Israel kutua ili kuhamisha maiti na majeruhi, wapiganaji wa Palestina walifyatua roketi jingine kuipiga helikopta hiyo.

Baadhi ya vituo vya habari vya lugha ya Kiebrania vimetangaza kwamba ingawa jeshi la Israel linadai ni wanajeshi watatu tu walioangamizwa, lakini dalili zote zinaonesha kuwa idadi ya waliouawa ni kubwa.

Baada ya kipigo hicho, wanajeshi wa Israel wameamrishwa kukimbia kwenye eneo hilo.