Pezeshkian: Kutumia mabavu na kulazimisha matakwa si kanuni ya mazungumzo
(last modified Wed, 04 Jun 2025 02:48:47 GMT )
Jun 04, 2025 02:48 UTC
  • Pezeshkian: Kutumia mabavu na kulazimisha matakwa si kanuni ya mazungumzo

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa Iran inakaribisha mazungumzo, lakini msingi wa mazungumzo ya kweli haupaswi kuwa kulazimisha matakwa au kutumia mabavu dhidi ya upande mwingine.

Masoud Pezeshkian, katika hafla ya kupokea hati za utambulisho kutoka kwa Balozi mpya wa New Zealand, Bethany Madden, iliyofanyika jana Jumanne, alimtakia mafanikio katika jitihada zake za kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili, na kusema:

“Dunia hii ni nyumba ndogo ya wanadamu ndani ya galaksi kubwa, na wote tunapaswa kujitahidi kuiweka kuwa mahali pa amani na utulivu badala ya vita na migogoro.”

Rais Pezeshkian amesema kuwa Iran iko tayari kuchukua hatua yoyote itakayosaidia kupanua ushirikiano na uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Akijibu kauli ya balozi mpya kuhusu matumaini ya kufanikiwa kwa mazungumzo yaisyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, alisema:

“Tumekuwa tukikaribisha mazungumzo, lakini mazungumzo halisi yanapaswa kujengwa juu ya kuheshimiana, sio juu ya vitisho na kulazimisha upande mwingine kukubali matakwa ya upande mmoja.”

Ameongeza kuwa: “Haiwezi kukubalika kwamba utawala fulani katika eneo hili, kwa msaada wa mataifa yenye nguvu, ufanye uhalifu wa kila aina, kisha uwalaumu wengine kuwa ndiyo wanaovuruga amani ya eneo hili ili tu kutumia hali hiyo kulazimisha matakwa yao. Rais Pezeshkian pia amesema: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mara nyingi imeeleza kuwa haina nia ya kutengeneza silaha za nyuklia, na daima iko tayari kushirikiana kwa uwazi ili kuthibitisha kauli hiyo.”

Kwa upande wake, Balozi mpya wa New Zealand, Bi Bethany Madden, ameshukuru kwa ukarimu na urafiki alioupokea tangu kuwasili kwake Tehran, na kusema:

“Nina matumaini makubwa na dhamira ya dhati ya kuchangia kikamilifu katika kuimarisha uhusiano kati ya New Zealand na Iran.”

Pia amezungumzia msimamo wa New Zealand kuhusu hali ya Gaza na kusema:

“New Zealand mara kadhaa imetoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja huko Gaza, na imeeleza wasiwasi wake kuhusu vikwazo vya kupeleka misaada ya matibabu na chakula kwa wakazi wa eneo hilo.”