Araghchi akiwa India: Iran inataka mvutano upungue kwani eneo linahitaji amani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i126152-araghchi_akiwa_india_iran_inataka_mvutano_upungue_kwani_eneo_linahitaji_amani
Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, amesema kuwa Tehran inazitaka India na Pakistan kujizuia na kuepusha kuongezeka kwa mvutano katika eneo hilo.
(last modified 2025-05-08T07:31:21+00:00 )
May 08, 2025 07:31 UTC
  • Araghchi akiwa India: Iran inataka mvutano upungue kwani eneo linahitaji amani

Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, amesema kuwa Tehran inazitaka India na Pakistan kujizuia na kuepusha kuongezeka kwa mvutano katika eneo hilo.

Araghchi ameyasema haya alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili mjini New Delhi siku ya Alhamisi, wakati ambapo mvutano unaongezeka baina ya nchi hiyo na jirani yake Pakistan kufuatia shambulio la mauaji lililotokea Kashmir.

Amesema: "Tunataka kupunguza mvutano katika eneo hili, hasa kwa ajili ya kukuza ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi za eneo."

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu nchini Iran amebainisha kwamba atajadili matukio ya hivi karibuni katika eneo katika mkutano na waziri mwenzake wa India.

Majeshi ya India na Pakistan yalifyatuliana mizinga katika mpaka unaozozaniwa mapema Jumatano, baada ya India kutekeleza "Operesheni Sindoor," ambayo ilijumuisha mfululizo wa mashambulizi ya makombora yaliyolenga maeneo ndani ya Pakistan na Kashmir inayosimamiwa na Pakistan.

Takriban raia 31 waliuawa na wengine 46 kujeruhiwa katika mashambulizi ya anga ya India na mashambulizi ya mipakani yaliyofuata katika Pakistan na Kashmir inayosimamiwa na Pakistan.

Pakistan nayo imesema imeangusha ndege tano za kivita za India katika mapigano hayo. Araghchi amesema kuwa katika ziara yake New Delhi atashiriki katika tume ya pamoja ya kiuchumi kati ya nchi mbili.

Ameongeza kuwa: "Ziara hii imepangwa kwa muda mrefu, na ilikuwa imepangwa kwamba tume hii iweze kufanyika."

Amebainisha kuwa pande zote zitapitia ushirikiano wa kiuchumi wa pande mbili, ambao ni muhimu sana.

Aidha amesema: "Wakati huo huo, tumekuwa na mashauriano ya kisiasa na India kila mara kuhusu masuala ya kikanda na kimataifa."

Araghchi alisafiri kuelekea India baada ya ziara ya siku moja nchini Pakistan, ambako alifanya mazungumzo na maafisa waandamizi wa nchi hiyo.