Araqchi: Awamu ya nne wa mazungumzo na Marekani imekuwa makini zaidi kuliko nyingine
Baada ya kumalizika duru ya nne ya mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati ya Iran na Marekani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "Mazungumzo hayo yalikuwa mazito zaidi, yenye umakini zaidi, yaliyo wazi zaidi na yanayoangalia mbele zaidi kuliko duru tatu zilizopita."
Vilevile Sayyid Abbas Araghchi amesema baada ya duru ya nne ya mazungumzo hayo mjini Muscat Oman kuwa: "Tunaweza kusema kwamba mazungumzo hayo yalikuwa mazito na ya wazi zaidi kuliko duru tatu zilizopita."
Ameongeza kuwa: "Katika awamu ya mara hii ya mazungumzo, tumeondoka kwenye maeneo ya jumla na tumeingia katika masuala mahususi. Ni wazi kwamba katika hali hiyo, mazungumzo yanakuwa magumu."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kwa kusema: "Majadiliano yenye manufaa sana yamefanyika na pande zote mbili sasa zinaelewa vyema misimamo ya kila mmoja wao. Katika duru hii ya mazungumzo, vipengele vingi vya masuala yanayobishaniwa vimefafanuliwa na misimamo imekaribiana kwa kiasi fulani. Tumeondoka na matumaini ya kusonga mbele zaidi."
Akisisitiza kuwa pande hizo mbili zimedhamiria kuendelea na mazungumzo, Araghchi amesema: "Makubaliano yamefikiwa kwa ajili ya mkutano ujao, lakini tarehe na mahali ni mambo ambayo yatatangazwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman. Nadhani wamu ya tano itafanyika wiki nyingine tofauti."
Duru ya nne ya mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Marekani ilifanyika jana Jumapili, Mei 11, 2025, Muscat, mji mkuu wa Oman, kwa muda wa saa tatu.