Kwa nini vikosi vya usalama vya Ufaransa vimefukuzwa Algeria?
Sambamba na kuongezeka mvutano kati ya Algeria na Ufaransa, serikali ya Algiers imechukua uamuzi wa kuwafukuza maafisa wawili wa kiintelijensia wa Ufaransa waliokuwa na pasipoti za kidiplomasia.
Serikali ya Algeria imewataja maafisa hao kuwa, "watu wasiofaa".
Katika miezi ya hivi karibuni, uhusiano kati ya Algeria na Ufaransa umeingia tena katika mgogoro kiasi kwamba, uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili pia umeathiriwa na hali hiyo ambapo idadi ya wanadiplomasia kutoka nchi hizo mbili wamefukuzwa, jambo ambalo lina mizizi katika historia ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Waalgeria katu hawawezi kusamehe au kusahau uhalifu wa Ufaransa katika nchi hiyo ya Kiafrika, hasa kwa kuwa maafisa wa Ufaransa kamwe hawajaomba msamaha wala kulipa fidia kwa Waalgeria. Ingawa Ufaransa imefanya uhalifu mkubwa zaidi na mauaji ya kimbari nchini Algeria, na nyaraka za kihistoria za uhalifu huu zinathibitisha hilo, lakini maafisa wa Paris daima wamekuwa wakikwepa kuomba radhi na badala yake wamekuwa wakitaka kuweko utendaji wenye mtazamo wa mustakabali.
Pamoja na hayo, katika miezi ya hivi karibuni hatua za kichochezi na sera za Ufaransa zimeamsha hasira ya muda mrefu ya Waalgeria na mzozo kati ya nchi hizo mbili umeongezeka na kushika kasi.
Hii ni mara ya pili ndani ya mwezi mmoja ambapo Algeria inawafukuza maafisa na wanadiplomasia wa Ufaransa. Algeria inadai kuwa Ufaransa inatumia kinga ya kidiplomasia kufuatilia malengo yake ya kijasusi katika ardhi ya nchi hiyo na maafisa hao wawili waliotimiliwa walikuwa makachero wa Shirika la Kijasusi la Ufaransa nchini Algeria.

Takriban mwezi mmoja uliopita, Algeria iliwafukuza wafanyakazi 12 wa ubalozi na balozi ndogo za Ufaransa. Hatua hii ilichukuliwa kama jibu kwa kile kilichoelezwa kuwa kuingilia kati kwa njia isiyokubalika na iliyozidi majukumu ya kidiplomasia.
Mzozo wa Algeria na Ufaransa unaongezeka wakati ambapo Ufaransa sio tu inapuuzilia mbali historia yake ya kikoloni huko Algeria bali pia katika miezi ya hivi karibuni imechukua hatua ambazo zimeongeza hasira ya Waalgeria. Kutambua utawala na mamlaka ya Morocco kwa Sahra ya Magharibi na kuandaa mazoezi ya pamoja ya kijeshi na Morocco ni miongoni mwa hatua hizo.
Katika muktadha huu pia, kunaweza kutajwa kukamatwa na kuhukumiwa kwa mwandishi wa Kifaransa-Algeria "Boualem Sansal" ambaye Ufaransa imesema kukamatwa kwake ni ukiukaji wa uhuru wa kujieleza nchini Algeria, wakati ambapo Algeria imemhukumu mwandishi huyo kwa tuhuma za "kutishia usalama wa taifa" na kumfunga gerezani miaka mitano.
Pia, nchi hizo mbili zina tofauti nyingi kuhusu wahamiaji. Ufaransa inailaumu Algeria kwa kutoshirikiana katika kurejesha raia wasio halali. Kwa upande mwingine, Algeria imekosoa uamuzi wa Ufaransa wa kupitia upya makubaliano ya uhamiaji ya mwaka 1968 na kuita kuwa ni tishio kwa uhusiano wa pande mbili.
Licha ya tofauti zote za kisiasa na mabadiliko ya kisiasa, kijamii na kimataifa, Ufaransa bado inaona Algeria kama eneo lake la ushawishi na katika miaka ya hivi karibuni imekuwa na uwepo katika nchi hii kwa njia mbalimbali, kiasi kwamba licha ya mizozo yote ya kisiasa, Ufaransa bado inajaribu kubaki kama mmoja wa washirika wakubwa wa kibiashara wa Algeria; lakini uhusiano huu wa kiuchumi pia umeathiriwa na masuala ya kisiasa na kihistoria.

Katika muktadha huu, hivi karibuni Baraza la Kuhuisha Uchumi la Algeria, ambalo linahesabiwa kuwa shirika kubwa zaidi la waajiri wa Algeria, lilifuta mkutano ambao ulipangwa kufanyika Ufaransa kwa ushiriki wa wanachama wa chama cha waajiri wa nchi hiyo. Hii ni licha ya kwamba kuwepo kwa mifarakano yoyote katika mahusiano kati ya nchi hizo mbili kunaweza kuathiri uagizaji wa bidhaa, nishati, kubadilishana wanafunzi na masuala ya uhamiaji katika muda mrefu na kushadidisha mvutano. Vilevile, kuendelea kwa mvutano huu kutasababisha kukosekana uthabiti katika ushirikiano wa kiusalama, na matokeo yake ni hatari ya shughuli za makundi ya kigaidi kwenye eneo la Sahel na Afrika Kaskazini.
Baadhi ya wachambuzi katika eneo hili wameonya kwamba, matukio na mvutano wa sasa kati ya nchi hizo mbili yanaweza kusababisha kukatwa kikamilifu uhusiano wa kidiplomasia kati ya Paris na Algies. Gazeti la Burkina Faso la Le Pays, limeandika: Hakika hakuna kitu kinachoweza kurekebishwa kati ya Paris na Algiers kwani wakati nchi hizi mbili zinapochukua hatua moja kuelekea utulivu au kupunguza mvutano, huchukua hatua mbili kuelekea kuongezeka kwa mgogoro.