Iran kujiunga na safu ya watengenezaji wa ndege za kibiashara duniani
Sambamba na maendeleo ya mradi wa uundaji wa ndege ya kwanza ya jet ya Iran ya kubeba abiria 8, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi karibuni itajiunga na kundi dogo la watengenezaji wa ndege za kibiashara duniani.
Hossein Shokri, Katibu wa Makao Makuu ya Maendeleo ya Uchumi wa Maarifa ya Anga nchini, ametangaza kuwa mradi wa uundaji wa jet ya kwanza ya abiria 8 umepiga hatua za maendeleo kwa asilimia 60 ya na kusema: "Sampuli za awali za sehemu mbalimbali za ndege hiyo, ikiwa ni pamoja na umbo la ndege yenyewe (fuselage), muundo wa mbawa, na mifumo ya kisasa ya avionics, zimezinduliwa katika maonyesho ya Kish Air Show."
Miongoni mwa sifa za ndege hiyo ya jet ya Iran ni uwezo wake wa kuruka katika viwanja vidogo vya ndege, uwezo wa kubeba abiria 8 na wahudumu 2 wa ndege, kusafiri masafa ya kilomita 2,500 kwa kasi ya kilomita 700 kwa saa, matumizi mazuri ya mafuta ya lita 350 kwa saa na mifumo ya kisasa ya urambazaji kulingana na viwango vya kimataifa.
Hossein Shokri ameashiria ushirikiano wa makampuni 15 katika mradi huo na kusisitiza kuwa: "Asilimia 45 ya vipuri, ikiwa ni pamoja na fuselage, mbawa na mifumo ya udhibiti wa ndege, imezalishwa ndani ya nchi, na kuhusu sehemu nyingine muhimu kama injini, tuna ajenda na ushirikiano wa kimataifa na nchi marafiki."
Kwa mujibu wa mipango iliyopo, safari ya kwanza ya majaribio ya ndege hiyo inatarajiwa katika nusu ya pili ya mwaka huu wa 1404 Hijria Shamsia.