OPEC: Mapato ya mauzo ya mafuta ya Iran yaongezeka kwa 14%
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i128808
Iran imefanikiwa kuongeza kwa kiasi kikubwa mapato yake ya mauzo ya mafuta mwaka uliopita. Hayo ni kwa mujibu wa takwimu mpya kutoka Shirika la Nchi Wazalishaji wa Mafuta Duniani (OPEC), zikionesha kuwa vikwazo vya Marekani havijafaulu kuzuia biashara ya mafuta nchini.
(last modified 2025-07-27T07:07:57+00:00 )
Jul 27, 2025 07:07 UTC
  • OPEC: Mapato ya mauzo ya mafuta ya Iran yaongezeka kwa 14%

Iran imefanikiwa kuongeza kwa kiasi kikubwa mapato yake ya mauzo ya mafuta mwaka uliopita. Hayo ni kwa mujibu wa takwimu mpya kutoka Shirika la Nchi Wazalishaji wa Mafuta Duniani (OPEC), zikionesha kuwa vikwazo vya Marekani havijafaulu kuzuia biashara ya mafuta nchini.

Ripoti ya Jumamosi iliyotolewa na Wizara ya Mafuta ya Iran, ikinukuu takwimu za OPEC, inaonesha kuwa Iran iliuza mafuta ghafi yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 46.776 mwaka 2024 ikiwa ni ongezeko la asilimia 13.62 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa Iran ndiyo nchi iliyoshuhudia ongezeko kubwa zaidi la mapato ya mauzo ya mafuta miongoni mwa wanachama 12 wa OPEC mwaka huo.

Ongezeko hilo lilijiri licha ya kushuka kwa jumla ya mapato ya mauzo ya mafuta ya OPEC, ambapo jumuiya hiyo iliona mapato yake yakipungua kutoka dola bilioni 678 mwaka 2023 hadi dola bilioni 652 mwaka 2024.

Saudi Arabia, ambayo ni muuzaji mkubwa zaidi wa mafuta duniani na kinara wa uzalishaji ndani ya OPEC, iliripoti kupungua kwa dola bilioni 24 katika mauzo yake, yakifikia dola bilioni 223.

Takwimu zinaonesha kuwa mapato ya mauzo ya mafuta ya Iran yamekaribia kuongezeka mara mbili ndani ya kipindi cha miaka mitatu hadi kufikia 2024.

Licha ya kuwepo kwa vikwazo vikali vya Marekani vinavyolenga wanunuzi wa mafuta ya Iran, nchi hii imeendelea kuongeza mauzo yake ya mafuta kwa kasi. Tangu kiwango cha chini cha kihistoria cha chini ya mapipa 300,000 kwa siku mwaka 2019, Iran sasa inauza zaidi ya mapipa milioni 1.8 kwa siku katika miezi ya hivi karibuni.

Hii ni pamoja na hatua za Marekani kutangaza awamu kadhaa za vikwazo dhidi ya mauzo ya mafuta ya Iran na washirika wake wa kimataifa, kwa lengo la kupunguza mauzo hayo hadi chini ya mapipa 100,000 kwa siku.