Araqchi atahadharisha kuhusu njozi za "Israel Kubwa" kabla ya mkutano wa dharura wa OIC
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi ametahadharisha kuwa kuwepo njozi za "Israel Kubwa" kunawakilisha hatari na tishio kubwa kwa amani na usalama wa dunia. Araqchi amezitolea wito nchi za Kiislamu kuchukua hatua za pamoja kukabiliana na ajenda ya kujitanua ya Israel.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameandika katika makala iliyochapishwa na gazeti la Asharq al Awsat kabla ya kufanyika Mkutano wa Dharura wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kwamba: Mkutano ujao unapasa kuwa hatua ya mageuzi ya kuimarisha azimio la pamoja la mataifa ya Kiislamu.
Amezihimiza nchi wanachama kukomesha "matamanio yasiyotosheka" ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na kukomesha mauaji, uharibifu na unyakuzi wa ardhi za Kiislamu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: Mkutano ujao wa Mawaziri wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) haupasi kuishia tu katika kutoa matamko ya mshikamano na watu wa Palestina au kueleza kusikitishwa nahali ya sasa.
Sayyid Abbas Araqchi ameutaja mkutano ujao wa OIC kuwa ni "mtihani wa kihistoria kwa Umma wa Kiislamu na labda mojawapo ya fursa chache za kuunda muungano wa kikanda na kimataifa ili kukomesha uvamizi wa Israel."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amehoji : "Ni nchi gani itakayolengwa baada ya Syria?" Ameonya kuwa matamshi na vitendo vya hivi karibuni vya Netanyahu si madai matupu bali ni tamko la moja kwa moja la sera na mkakati unaolenga kutekeleza wazo la "Israel Kubwa kutoka Mto Nile hadi Euphrates."