Pezeshkian amwambia Putin: Iran haijawahi kamwe kutaka kumiliki silaha za nyuklia
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana Jumatatu alizungumza kwa simu na Rais Vladimir Putin wa Russiai na kumweleza kuwa Tehran haijawahi kutaka kumiliki wala haitatafuta silaha za nyuklia, akisisitiza msimamo wa muda mrefu wa Iran kuhusu mpango wake wa nyuklia.
Rais Pezeshkian ameishukuru Moscow kwa kuunga mkono haki ya Iran ya kurutubisha madini ya urani na kusema: Sera ya nyuklia ya nchi inatokana misingi ya kidini na kiulinzi. "
"Iran haijawahi kutaka kumiliki, haitaki na wala haina lengo la kuunda silaha za nyuklia kwa kuzingatia imani na doktrini yake ya kiulinzi," amesema Rais wa Iran.
Katika mazungumzo hayo ya simu, Rais Vladimir Putin wa Russia ameuelezea uhusiano wa nchi yake na Iran kuwa imara na unaoimarika kwa kasi na kuongeza kuwa biashara kati ya pande mbili imeongezeka kwa asilimia 11 katika nusu ya kwanza ya mwaka huu na kwamba ushirikiano wa Moscow na Tehran katika miradi mikubwa ukiwemo mradi wa ujenzi wa reli ya Rasht- Astara unapiga hatua.
Putin pia alimueleza Pezeshkian kuhusu mazungumzo yake ya hivi karibuni na Rais wa Marekani Donald Trump huko Alaska. Rais wa Russia amesema majadiliano yake na Trump yalijikita katika kadhia ya Ukraine na kwamba matokeo mazuri yamepatikana, ambayo yanaweza kusaidia kutatua mzozo huo iwapo yatatekelezwa kikamilifu.