Polisi ya Iran yaangamiza magaidi 8 waliohusika na shambulizi la kigaidi Sistan na Baluchestan
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i130062-polisi_ya_iran_yaangamiza_magaidi_8_waliohusika_na_shambulizi_la_kigaidi_sistan_na_baluchestan
Polisi ya Iran imetoa kipigo kikubwa kwa magaidi wanaoungwa mkono na nchi ajinabi katika mkoa wa Sistan na Baluchestan, kusini-mashariki mwa Iran, kwa kuwaangamiza magaidi 8 waliohusika na shambulio baya la karibuni dhidi ya maafisa wa polisi katika mkoa huo.
(last modified 2025-08-27T10:46:22+00:00 )
Aug 27, 2025 10:46 UTC
  • Polisi ya  Iran yaangamiza magaidi 8 waliohusika na shambulizi la kigaidi Sistan na Baluchestan

Polisi ya Iran imetoa kipigo kikubwa kwa magaidi wanaoungwa mkono na nchi ajinabi katika mkoa wa Sistan na Baluchestan, kusini-mashariki mwa Iran, kwa kuwaangamiza magaidi 8 waliohusika na shambulio baya la karibuni dhidi ya maafisa wa polisi katika mkoa huo.

Saeed Montazer al Mahdi, msemaji wa Polisi ya Iran ameeleza kuwa askari wao kutoka kikosi cha FARAJA pamoja na wenzao kadhaa wa intelijinsia leo Jumatano wametekeleza kwa mafanikio oparesheni dhidi ya magaidi hao na kuwaangamiza wote.

Idadi kubwa ya silaha na zana za kijeshi zimenaswa kutoka kwa magaidi hao waliouawa. 

Tarehe 22 mwezi huu wa Agosti askari watano wa Iran waliuawa katika shambulio la kigaidi. Magaidi walivishambulia vituo viwili vya doria vya polisi katika eneo la Daman katika Kaunti ya Iranshahr wakati polisi hao walipokuwa zamu.

Kundi la kigaidi linalojiita Jaishul Adl limedai kuhusika na hujuma hiyo dhidi ya polisi. 

Uhalifu huo ulifuatia shambulio lingine baya la kigaidi mnamo Julai 26, wakati magaidi watatu waliokuwa na silaha kutoka kundi la wanamgambo wa Jaishul Adl waliposhambulia Mahakama ya mkoa wa Sistan na Balouchestan huko Zahedan.

Raia sita waliuliwa shahidi akiwemo mama na mwanaye wa miezi sita, na wengine 24 walijeruhiwa katika shambulio hilo la makusudi dhidi ya raia. 

Mkoa wa Sistan na Baluchestan ambao unapakana na Pakistan, umekuwa ukikumbwa na  mashambulizi  kigaidi dhidi ya raia na askari usalama.

Makundi ya kigaidi yanayotekeleza mashambulizi dhidi ya maslahi ya Iran katika maeneo ya kusini mashariki na kusini magharibi mwa nchi yanaaminika kuwa na uhusiano na mashirika ya kijasusi ya kigeni.