Iran yakosoa uamuzi wa Australia wa kupunguza kiwango cha uhusiano wa nchi hizi mbili
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i130090-iran_yakosoa_uamuzi_wa_australia_wa_kupunguza_kiwango_cha_uhusiano_wa_nchi_hizi_mbili
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imechapisha taarifa ikiutaja uamuzi wa serikali ya Australia wa kupunguza kiwango cha uhusiano wa kidiplomasia na Iran kuwa kinyume na utamaduni wa uhusiano mkongwe wa nchi hizi mbili.
(last modified 2025-08-28T04:18:48+00:00 )
Aug 28, 2025 04:18 UTC
  • Iran yakosoa uamuzi wa Australia wa kupunguza kiwango cha uhusiano wa nchi hizi mbili

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imechapisha taarifa ikiutaja uamuzi wa serikali ya Australia wa kupunguza kiwango cha uhusiano wa kidiplomasia na Iran kuwa kinyume na utamaduni wa uhusiano mkongwe wa nchi hizi mbili.

Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema: "Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaeleza masikitiko yake kuhusu suala hili na inalichukulia ombi la serikali ya Australia la kutaka balozi na wanadiplomasia kadhaa wa Iran waondoke nchini humo kuwa halina uhalali wa kisheria na ni kinyume cha uhusiano wa jadi wa kidiplomasia baina ya nchi mbili."

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran inakanusha kikamilifu tuhuma zilizotolewa dhidi ya Iran kuwa inachochea chuki dhidi ya Mayahudi na kuitaka serikali ya Australia izingatie ukweli wa kihistoria kwamba suala zima la chuki dhidi ya Uyahudi kimsingi ni jambo lililoanzia Ulaya na nchi za Magharibi ambalo limejitokeza katika nchi hizo kwa namna na nyakati tofauti. Pamoja na hayo, katika miaka ya hivi karibuni, suala hili limekuwa likitumika vibaya kwa ajili ya kukandamiza maandamano yoyote dhidi ya uvamizi, ubaguzi wa rangi na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.

Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelaani uamuzi wa Australia wa kumfukuza balozi wa Tehran nchini humo kutokana na madai eti ya mashambulizi kwenye vituo vya Kiyahudi, na kueleza kuwa ni kitendo cha kutaka kuiridhisha "serikali inayoongozwa na wahalifu wa kivita."

Katika ujumbe wake uliochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X  Jumanne, Abbas Araqchi alipinga madai ya Canberra, akiashiria ulinzi wa muda mrefu wa Iran kwa jamii ya Mayahudi hapa nchini.

"Iran ni nyumbani kwa moja ya jamii kongwe zaidi za Mayahudi duniani, ikiwa ni pamoja na makumi ya masinagogi. Kuishutumu Iran kuwa imeshambulia vituo kama hivyo nchini Australia, wakati sisi wenyewe tunafanya kila tuwezalo kuvilinda katika nchi yetu, hakuna maana yoyote," amesema Abbas Araqchi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema "Iran inalipa gharama ya uungaji mkono wa watu wa Australia kwa Palestina", akimaanisha kuongezeka kwa maandamano ya kuitetea na kuiunga mkono Palestina kote nchini Australia kufuatia vita vya Israel dhidi ya watu wa Gaza.