Haj Ali Akbari: Ufaransa, Ujerumani na Uingereza ni watumishi wa Wazayuni
Imamu wa muda wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran amekosoa vikali hatua ya hivi karibuni ya mataifa matatu ya Ulaya dhidi ya Iran, akiitaja kuwa ni haramu, ya kisiasa na iliyotekelezwa kwa mashinikizo ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Amesisitiza kuwa nchi hizo zimejivunjia heshima kwa kujitwika jukumu la kuhudumia utawala wa Kizayuni wa Israel, na kuongeza kuwa taifa la Iran litavuka mitihani hii kwa uthabiti.
Hujjatul Islam wal-Muslimin Haj Ali Akbari, khatibu wa muda wa swala ya Ijumaa mjini Tehran, katika hotuba yake ya leo ameongeza kuwa: “Hatua hii ni haramu, isiyo ya kimaadili na ya kisiasa kabisa, iliyochochewa na mashinikizo kutoka Marekani na makundi ya ushawishi ya Kizayuni. Imebainika wazi kuwa Ulaya imegeuka kuwa chombo cha utawala wa Kizayuni. Wanajaribu kufunika fedheha ya kushindwa kwa Marekani na Israel katika vita vyao vya karibuni dhidi ya Iran, lakini kwa hakika wamejifedhehesha zaidi. Iran imetekeleza ahadi zake zote na hata imefanya zaidi ya ilivyotarajiwa."
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Hujjatul Islam wal-Muslimin Haj Ali Akbari ametoa rambirambi kwa mnasaba wa siku za kukumbuka kuuawa shahidi Imam Hassan Askari (AS) na pongezi kwa kuanza kwa uongozi wa Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu Aharakishe Kudhihiri Kwake).
Amesema kuwa kipindi hiki ni fursa ya kuhuisha ahadi na uaminifu kwa Imam wa Zama, na kuongeza kuwa: “Tunatumaini kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, sote tutafaidika na dua njema na baraka zake.”
Aidha ameangazia umuhimu wa taqwa, akisema kuwa kulinda hazina za kiroho na kijamii ni miongoni mwa alama kuu za taqwa. Ameongeza kuwa waumini katika miezi miwili iliyopita wameonyesha mapenzi makubwa kwa Bwana wa Mashahidi, Imam Hussein (AS), na wamepata hazina kubwa ya nuru, ambayo ilidhihirika kwa upeo katika matembezi na Ziyara ya Arubaini. Amesema ni jukumu letu sote kuomba msaada wa Mwenyezi Mungu ili tuweze kuhifadhi hazina hii ya kiroho.
Hujjatul Islam wal-Muslimin Haj Ali Akbari pia amegusia kuwasili kwa mwezi wa Rabi’ul Awwal, akieleza kuwa mwezi huu una upekee wake kwa sababu ni mwezi wa kukumbuka kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) na Imam Sadiq (AS).