Hamas: Israel imeshindwa kufikia malengo yake kupitia mauaji ya kimbari
Harakati ya Kiislamu ya Mapambano ya Ukombozi wa Palestina, Hamas, limesisitiza kuwa utawala wa Israel umeshindwa kufanikisha malengo yake kupitia vita vya zaidi ya miaka miwili vya mauaji ya kimbari dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Kiongozi mwandamizi wa Hamas na mkuu wa mazungumzo, Khalil al-Hayya, aliambia televisheni ya Al Jazeera ya Qatar siku ya Jumamosi kwamba: “Mvamizi ameshindwa kufikia malengo yake baada ya zaidi ya miaka miwili ya vita.”
Kauli hiyo ilihusiana na malengo ya utawala wa Kizayuni ya kutaka kuuteka Ukanda wa Gaza na kuwafukuza wakazi wake zaidi ya milioni mbili, kufuatia mauaji ya kimbari yaliyoanza Oktoba 2023.
Tel Aviv ilianzisha vita hivyo kama jibu kwa operesheni ya kihistoria ya harakati ya Hamas ambayo ilisababisha wanajeshi na raia kadhaa wa Kizayuni kunaswa mateka.
Wakati huohuo, utawala huo ulidai kuwa vita hivyo vya kinyama vililenga pia kuwarudisha mateka hao, lakini nao ukashindwa kutimiza lengo hilo.
Mapema mwezi huu , Hamas na utawala wa Israel walifikia makubaliano kupitia mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yaliyofanyika nchini Misri.
Makubaliano hayo yamepanga utekelezaji wa awamu ya kwanza ya usitishaji mapigano, kulingana na mpango wa vipengele 20 uliowasilishwa na Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye alisema mpango huo unalenga “kumaliza mauaji ya kimbari.”
Al-Hayya alinukuu Trump akisema kuwa “vita vimekwisha,” na kuongeza kuwa maafisa wa Marekani wamekuwa wakitoa kauli kama hizo karibu kila siku.
Hata hivyo, alionya kuhusu namna Isareli ianvyovunja makubaliano ikiwemo kuzuia kuingia kwa baadhi ya bidhaa na misaada muhimu ndani ya Gaza, na kuongeza kuwa “Ni kana kwamba bado tupo katikati ya vita.”
Alisema pia:“Hali ya kibinadamu inatupa wasiwasi mkubwa, na mvamizi anaendelea kuzuia misaada kuingia Gaza.”
Kiongozi huyo wa Muqawama aliongeza kuwa Rais wa Marekani ana uwezo wa kuizuia Israel, na kwamba Hamas imeiambia Washington kuwa inataka utulivu wa eneo, na haitatoa visingizio kwa utawala huo “kuanzisha tena vita.”
Al-Hayya alibainisha kuwa Hamas itaendelea kutekeleza wajibu wake kwa kurudisha miili ya mateka wa Kizayuni waliokufa, licha ya ugumu wa kazi hiyo kutokana na uharibifu mkubwa uliofanywa na vita hivyo.
Aidha, amesema kuwa Hamas itaendelea kushikilia ahadi yake ya kukabidhi utawala wa Gaza kwa chombo cha Kipalestina, kwa mujibu wa makubaliano yaliyopo.