AU yahimiza kuchukuliwa hatua madhubuti za kudhamini chakula Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i132438-au_yahimiza_kuchukuliwa_hatua_madhubuti_za_kudhamini_chakula_afrika
Kamishna wa Kilimo, Maendeleo Vijijini, Uchumi wa Bluu na Mazingira Endelevu wa Umoja wa Afrika (AU), Moses Vilakati ametaka kuchukuliwe juhudi zaidi na zilizoratibiwa vyema kwenye bara zima la Afrika ili kushughulikia changamoto kubwa za usalama wa chakula barani humo.
(last modified 2025-10-26T12:00:22+00:00 )
Oct 26, 2025 12:00 UTC
  • AU yahimiza kuchukuliwa hatua madhubuti za kudhamini chakula Afrika

Kamishna wa Kilimo, Maendeleo Vijijini, Uchumi wa Bluu na Mazingira Endelevu wa Umoja wa Afrika (AU), Moses Vilakati ametaka kuchukuliwe juhudi zaidi na zilizoratibiwa vyema kwenye bara zima la Afrika ili kushughulikia changamoto kubwa za usalama wa chakula barani humo.

Ametoa mwito huo wakati wa mkutano wa mawaziri wa AU wa kila baada ya miaka miwili. Mkutano huo umefanyika kama sehemu ya Kikao cha 6 cha Kawaida cha Kamati Maalumu ya Kiufundi ya Kilimo, Maendeleo Vijijini, Maji na Mazingira katika makao makuu ya AU huko Addis Ababa, Ethiopia.

Mkutano huo wa ngazi ya juu wa mawaziri umewaleta pamoja mawaziri na wataalamu kutoka kote barani Afrika wanaohusika na kilimo, mifugo, uvuvi, maendeleo ya vijijini, maji na usafi wa mazingira sambamba na mabadiliko ya hali ya hewa.

Akihutubia mkutano huo,  Moses Vilakati amesema kwamba majanga ya asili yanayoongezeka na yanayojirudia yanaathiri mamia ya mamilioni ya watu kote barani Afrika na kusababisha hasara za kiuchumi zinazofikia mabilioni ya dola.

Amesema: "Uzalishaji wa kilimo barani Afrika bado unabaki chini ya wastani, hasa kutokana na matumizi madogo ya pembejeo zinazoongeza tija kama vile mbolea, umwagiliaji na mbegu bora, pamoja na mbinu bora za kilimo." Kamishna huko wa AU katika masuala ya kilimo amesisitiza pia kwamba kushughulikia changamoto hizo kitaasisi ni "muhimu sana katika kufungua uwezo wa kupatikana mapinduzi ya kilimo na chakula barani Afrika."

Vilevile ametoa pongezi kwa maendeleo yanayostahili kupongezwa yaliyopatikana katika baadhi ya maeneo ya Afrika katika kuimarisha sekta ya kilimo-chakula na kusema kwamba kazi iliyoko mbele ya bara la Afrika bado ni kubwa. Amesema mpango wa kilimo-chakula unazingatia maeneo muhimu ikiwa ni pamoja na afya ya udongo, uboreshaji wa mbolea, maendeleo ya mifumo ya mbegu na kutoa fursa za ajira kwa vijana.