Zimbabwe yatoa mwito wa kuondolewa vikwazo vya Magharibi bila ya masharti
Jana Zimbabwe ilifanya maadhimisho ya Siku ya Kikanda ya Kupinga Vikwazo huko Harare, mji mkuu wa nchi hiyo. Wananchi wa Zimbwe wametaka kuondolewa vikwazo vya nchi za Magharibi bila ya masharti na kuruhusiwa taifa lao kufanikisha malengo yake ya ustawi wa kiuchumi.
Siku ya SADC ya Kupinga Vikwazo iliadhimishwa jana Oktoba 25 na ilianzishwa na Jumuiya hiyo ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ambayo ni jumuiya ya kikanda yenye wanachama 16. Siku hiyo ilitangazwa mwaka 2019 kama mpango wa pamoja wa kikanda wa kukemea vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Zimbabwe kufuatia mpango wa mageuzi ya ardhi wa nchi hiyo ambao uligawa ardhi kutoka kwa wakulima Wazungu wachache na kuwapa Waafrika wenye asili ya Zimbabwe. Katika hotuba yake katika maadhimisho hayo, Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe ametoa mwito wa kuondolewa kabisa na bila ya masharti vikwazo hivyo vya nchi za Magharibi, akisema kwamba nchi hiyo itaendelea kuwa imara katika maendeleo licha ya kuweko vikwazo hivyo haramu.
Rais Mnangagwa pia amesema kwamba "licha ya athari mbaya na changamoto nyingine kama vile ukame unaosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa na mambo ya dharura ya afya ya umma, lakini pamoja na hayo yote, uchumi wa taifa letu umeendelea kuwa katika mwelekeo mzuri wa ustawi." Vilevile amesema: Licha ya changamoto zinazotokana na vikwazo hivyo, nchi yetu bado imejitolea kufanya ushirikiano wa pande nyingi na kimataifa kwa ajili ya kupigania amani ya kimataifa, usalama, haki na kuweko usawa na uadilifu duniani.
Naye Martin Zharare, mkurugenzi mtendaji wa Citizens Against Economic Sanctions, kundi la kupambana na vikwazo huko Zimbabwe amesema kwenye maadhimisho hayo kwamba, vikwazo vinapaswa kuondolewa bila ya masharti kwani vinazuia ukuaji wa uchumi na ni kwa madhara ya watu wa kawaida.