Kwa nini mazungumzo na Marekani hayana maana?
Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wametoa sababu mbalimbali kwa nini mazungumzo na Marekani hayana natija.
Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wametoa sababu mbalimbali kwa nini mazungumzo na Marekani hayana natija. Sababu hizo zinatokana na uzoefu wa kihistoria, itikadi na uchambuzi wa tabia ya watawala wa Marekani.
Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kwamba Marekani huingia kwenye mazungumzo kwa mtazamo wa ubabe na ubeberu na haitafuti makubaliano ya haki, bali lengo lao ni kulazimisha matakwa yao dhidi ya wengine. Tabia hii ya viongozi wa Marekani inapingana na kanuni za ‘uhuru’ na ‘kupinga dhulma,’ ambazo ni msingi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Uzoefu wa huko nyuma, hasa katika mchakato wa mazungumzo ya nyuklia ya JCPOA, umebainisha wazi kwamba mazungumzo na Marekani sio tu kwamba hayatatui matatizo ya kiuchumi, bali watawala wa Marekani hutumia fursa hii kutekeleza sera zao zisizo za kibinadamu za kuongeza vikwazo dhidi ya Iran. Hali hii inaonyesha kwamba mazungumzo ni chombo cha Marekani kushadidisha mashinikizo na kujipatia faida bila kuzingatia upande wa pili. Aina hii ya mazungumzo sio tu haina matokeo bali inachukuliwa kuwa yenye madhara.
Watawala wa Marekani wakati wa mazungumzo ya JCPOA na baada ya hapo walitumia mazungumzo hayo kama zana ya kidiplomasia na kisheria kwa ajili ya kuongeza vikwazo dhidi ya Iran. Vitendo hivi, kwa maoni ya wachambuzi wengi na viongozi wa Iran, vinachukuliwa kama matumizi mabaya ya nafasi ya mazungumzo na makubaliano ya kimataifa. Licha ya Marekani kujiondoa rasmi katika JCPOA mwaka 2018, imejaribu kutumia utaratibu wa 'Snapback' katika Azimio la 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran.
Katika vipindi mbalimbali vya mazungumzo, Wamarekani, badala ya kupunguza mvutano, waliweka vikwazo vipya dhidi ya taasisi na watu binafsi wa Iran ili kuvitumia kama nguvu ya kushinikiza katika mazungumzo. Tabia hii ilipelekea Iran ipoteze imani na Marekani na kuibua changamoto katika mchakato wa mazungumzo.
Wakati Iran ilipofikia makubaliano na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) kwa ajili ya uwazi, Marekani na washirika wake wamepuuza makubaliano hayo kwa kuwezesha utaratibu wa 'Snapback' wa kurejesha vikwazo dhidi ya Iran. Viongozi wa Iran wanaichukulia tabia hii kama mfano wa “diplomasia ya hadaa” na “matumizi mabaya ya sheria za kimataifa.”

Mtazamo wa uhasama wa Marekani dhidi ya Iran sio tu haukupungua katika mchakato wa mazungumzo, bali watawala wa White House walitumia kila fursa kutekeleza vikwazo zaidi na kuweka vizuizi vya kiuchumi dhidi ya Iran. Sera hizi za uhasama dhidi ya Iran zilianza kutumika wakati ambapo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika miaka iliyopita ilitimiza ahadi zake zote katika JCPOA na kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, hivyo ni wazi kuwa ni upande wa pili ndio haukufungamana na ahadi zake.
Tabia ya unafiki ya Wamarekani katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Iran pia iliendelea, ambapo kinyume na kanuni za kidiplomasia na sheria za kimataifa, walishirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel katika vita vya siku 12 dhidi ya Iran. Uchokozi huo ulikiuka wazi sheria zote za kimataifa. Katika uchokozi huo, mbali na kuwaua makamanda wa kijeshi , wavamizi hao waliwaua kigaidi wanasayansi wa nyuklia na raia wa kawaida wakiwemo wanawake na watoto. Aidha wavamizi hao walilenga kwa mabomu vituo vya Iran vya shughuli za amanni za nyuklia. Mlolongo huu wa vitendo vya uhasama vya Ikulu ya White House, kwa maoni ya viongozi wa Iran, ni ishara ya ushirikiano katika uvamizi haramu wa kijeshi na ukiukaji wa sheria za kimataifa.
Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, akifafanua sababu ya kutokusalimu amri kwa taifa lenye heshima la Iran mbele ya mashinikizo na vitisho vya adui ambaye anataka Iran iache teknolojia muhimu ya kurutubisha madini ya urani yanayotumika katika sekta ya nyuklia, amesisitiza kuwa: “Mazungumzo ambayo Marekani tangu mwanzo imeainisha na kuamua matokeo yake, hayana maana na yana madhara, kwa sababu yanamshawishi adui jeuri kufuatilia malengo mengine. Mazungumzo hayo hayatupunguza madhara yoyote, na hakuna taifa lenye heshima na mwanasiasa mwenye busara atayakubali mazungumzo ya aina hii.”
Kwa mtazamo wa viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mazungumzo na Marekani sio tu hayana matokeo bali pia yana madhara. Sababu za mtazamo huu ni pamoja na ukiukaji wa ahadi wa mara kwa mara, matumizi ya mazungumzo kama chombo cha kufikia malengo haramu, ushirikiano katika vitendo vya uhasama vya utawala wa Kizayuni wa Israel na muundo jumla wa sera za Marekani ambao si wa kuaminika.