Timu ya voliboli ya wanawake ya Iran yatwaa ubingwa wa CAVA 2025
Timu ya voliboli ya wanawake ya Iran iliigaraza Uzbekistan kwenye mashindano ya Kombe la Chalenji ya Wanawake wa Asia ya Kati (CAVA) jana Jumapili na kushinda taji hilo la kieneo kwa mara ya kwanza katika historia.
Timu hiyo ya taifa ya Iran ya voliboli ya wanawake iliishinda Uzbekistan kwa seti za moja kwa moja za (25-14, 25-14, 25-19) katika mpambano huo wa fainali uliopigwa jana huko Tashkent, mji mkuu wa Uzbekistan.
Kabla ya hapo, timu hiyo ya voliboli ya wanawake ya Iran siku ya Ijumaa iliinyoa kwa chupa mwenyeji Uzbekistan katika duru ya awali ya mashindano hayo, gazeti la Tehran Times limeripoti.
Timu hiyo ya voliboli ya wanawake ya Iran iliishinda Uzbekistan kwa seti 3-0 (25-15, 25-14, 25-16) kwenye pambano hilo la Ijumaa.
Kikosi hicho kinachonolewa na mkufunzi Lee Do-hee hapo awali kilizishinda Kyrgyzstan na Tajikistan katika michuano hiyo ya kikanda ya CAVA.
Iran ilianza kampeni yake huko Tashkent kwa ushindi wa seti 3-0 dhidi ya Kyrgyzstan na kisha kuishinda Tajikistan kwa matokeo sawia.
Kombe la Chalenji ya Voliboli ya Wanawake ya CAVA ni mashindano ya kieneo ya voliboli kwa timu za kitaifa za wanawake ambazo ni wanachama wa Chama cha Voliboli cha Asia ya Kati, ikiwa ni bodi inayosimamia mchezo huo katika eneo la Asia ya Kati na Kusini.