Zarif: Uhusiano wa Iran na Oman unastawi katika nyanja zote
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu na Oman unaendelea kustawi katika nyanja zote.
Muhammad Javad Zarif, ameyasema hayo mbele ya waandishi wa habari akiwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Yusuf bin Alawi ambaye aliwasili hapa nchini mapema leo. Dakta Zarif amesema uhusiano wa Iran na Oman ni wa kupigiwa mfano na wa aina yake na kusisitiza kwamba hakuna kizuizi chochote katika kustawishwa uhusiano wa Tehran na Muscat.
Akiashiria azma ya Iran na Oman ya kuimarisha uhusiano baina yao, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, uhusiano biana ya nchi mbili hizi ni wa kupigiwa mfano; na Iran inawashukuru viongozi wa Oman akiwemo Sultan Qaboos kwa nafasi na mchango muhimu waliotoa katika utatuzi wa kadhia ya nyuklia.
Zarif aidha amesema Oman ni jirani mzuri na wa kuaminika kwa Iran na akaeleza matumaini aliyonayo, kwamba safari ya ujumbe wa ngazi za juu wa kisiasa na kiuchumi wa Oman hapa nchini utafungua ukurasa mpya wa kustawisha uhusiano wa kidugu na kirafiki baina ya Iran na Oman.
Katika mazungumzo hayo na waandishi wa habari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman amesema ushirikiano wa Tehran na Muscat umekuwa na taathira chanya kwa uhusiano wa kieneo na kimataifa.
Yusuf bin Alawi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman aliwasili mjini Tehran leo kwa lengo la kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa ngazi za juu wa Iran na kushauriana nao juu ya masuala muhimu ya pande mbili na ya kieneo.../