Kharrazi: Uadui wa Marekani kwa Iran si jambo jipya
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i53501-kharrazi_uadui_wa_marekani_kwa_iran_si_jambo_jipya
Mkuu wa Baraza la Kiistratijia la Uhusiano wa Nje la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, uadui wa Marekani dhidi ya Iran si jambo jipya na kwamba katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, dola hilo la kibeberu limekuwa likionesha uadui wake huo dhidi ya taifa la Iran kila inapopata fursa ndogo tu.
(last modified 2025-10-22T08:58:50+00:00 )
May 15, 2019 08:11 UTC
  • Kharrazi: Uadui wa Marekani kwa Iran si jambo jipya

Mkuu wa Baraza la Kiistratijia la Uhusiano wa Nje la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, uadui wa Marekani dhidi ya Iran si jambo jipya na kwamba katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, dola hilo la kibeberu limekuwa likionesha uadui wake huo dhidi ya taifa la Iran kila inapopata fursa ndogo tu.

Sayyid Kamal Kharrazi amesema hayo katika mahojiano na televisheni ya France 24 yaliyorushwa hewani usiku wa kuamkia leo na kuongeza kuwa,  Marekani imeiwekea Iran vikwazo vikubwa vya kiuchumi, lakini kamwe haitofanikiwa kufikia malengo yake kwani wananchi wa Iran wamepevuka vizuri sana kisiasa na wamesimama imara kukabiliana na vikwazo hivyo vya Marekani.

Amezungumzia pia harakati za kijeshi za Marekani katika eneo hili na kuongeza kuwa, kama Marekani itataka kuchukua hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya Iran basi ijue kuwa Iran iko tayari kabisa kutoa majibu ya uchokozi huo.

Pande zilizobakia katika mapatano ya JCPOA baada ya Marekani kujitoa

 

Vile vile amesema, madola ya Ulaya yanaweza kuonyesha nia na irada yao ya kutaka kuhifadhiwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kwa kutekeleza ahadi zake kama vile kutekelezwa haraka mfumo maalumu wa mabadilisho ya kifedha baina ya Ulaya na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran  kwa kifupi, INSTEX.

Mkuu huyo wa Baraza la Kiistratijia la Uhusiano wa Nje la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran  amebainisha sababu za uamuzi wa hivi karibuni wa Iran wa kusitisha baadhi ya ahadi zake kwa mujibu wa makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA na kueleza kuwa, uamuzi huo wa Tehran ni haki yake ambayo inatambuliwa na makubaliano hayo.