Meja Jenerali Baqeri: Majeshi ya Iran yako tayari kujibu uadui wowote ule
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i54648-meja_jenerali_baqeri_majeshi_ya_iran_yako_tayari_kujibu_uadui_wowote_ule
Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Iran amesema kuwa, majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yako tayari kujibu kwa nguvu zote uadui wowote ule dhidi yake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 09, 2019 03:55 UTC
  • Meja Jenerali Baqeri: Majeshi ya Iran yako tayari kujibu uadui wowote ule

Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Iran amesema kuwa, majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yako tayari kujibu kwa nguvu zote uadui wowote ule dhidi yake.

Meja Jenerali Muhammad Hossein Baqeri amesema hayo leo Jumanne katika sherehe za kumtambulisha kaimu mpya wa Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Iran na kusema kuwa Jamhuri ya Kiislamu haigopi vita ikilizimika kufanya hivyo ingawa haipendi vita. Ameongeza kuwa, majeshi ya Iran yako tayari kutoa majibu makali kwa uchokozi na uadui wowote itakaofanyiwa.

Meja Jenerali Baqeri amezungumzia jinsi Marekani na Ulaya zilivyoshindwa kutekeleza ahadi zao ndani ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kusisitiza kuwa, licha ya kwamba nchi za Magharibi zimekataa kutekeleza ahadi zao katika makubaliano hayo, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilivumilia kwa muda wa mwaka mzima na kutoa fursa kwa walimwengu na tawala zote duniani kupata yakini kwamba si Jamhuri ya Kiislamu iliyokuvunja ahadi zake ndani ya JCPOA.

Mabaki ya ndege ya kijasusi ya Marekani, Global Hawk iliyotunguliwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH baada ya kuingia katika anga ya Iran

 

Mkuu huyo wa Vikosi vya Ulinzi vya Iran vile vile amezungumzia jinsi Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH lilivyotungua ndege ya kijasusi ya Marekani Global Hawk katika anga ya Iran na kusema kuwa ushujaa huo wa jeshi la SEPAH umewastaajabisha walimwengu wote na kuwatia woga maadui hasa Marekani. 

Amesema kuwa, leo hii Iran imepiga hatua kubwa sana katika masuala ya ulinzi wa makombora, baharini, ardhini na angani na ni kwa sababu hiyo ndio maana maadui ambao wanategemea sana mashambulizi ya anga, waogope kuanzisha uadui wowote dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.