Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran: Marekani imechanganyikiwa na inatangatanga kimkakati
Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo mjini Tehran amesema, hatua ya Marekani ya kumwekea vikwazo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ni kitendo kisicho na maana, cha kitoto na cha kuchekesha na akasisitiza kuwa: Hatua hii ni ishara ya kuchanganyikiwa na kutangatanga kimkakati watawala wa Marekani.
Hujjatul Islam Mohammad Javad Haj Akbari ameeleza kuwa, ni jambo la fahari na la kujivunia kwa Waziri wa Mambo ya Nje na timu ya diplomasia ya Iran kuwekewa vikwazo na Marekani na akafafanua kwamba: Mwenendo huu wa serikali ya Marekani unaashiria kudhoofika na kuporomoka timu ya diplomasia na ile inayotawala nchi hiyo.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran amesema, mahubiri ya muqawama yametoa tija iliyokusudiwa na akabainisha kwamba: Hatua ya Marekani imeonyesha kuwa diplomasia ya kubembeleza haijaweza kuwa na tija kwa Washington na kwa hiyo nyoyo zao zitafarijika kwa kuchukua hatua kama hiyo.
Siku ya Jumatano, wizara ya fedha ya Marekani ilitangaza kuwa imeliweka jina la Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Zarif kwenye orodha yake ya vikwazo.
Akizungumzia hatua hiyo iliyochukuliwa na wizara ya fedha ya Marekani dhidi yake, Dakta Zarif amesema, sababu ya kuwekewa vikwazo ni hotuba na mahojiano anayofanya na mashirika ya habari ya Marekani, na akaandika katika ukurasa wake wa Twitter kwa kuhoji: Kwa ajili ya kusikia sauti yangu, kwani wananchi wa Marekani wanahitajia kibali cha wizara ya Marekani?!.../