Zarif: Iran inaunga mkono ushiriki chanya wa Syria na Umoja wa Mataifa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i55777-zarif_iran_inaunga_mkono_ushiriki_chanya_wa_syria_na_umoja_wa_mataifa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuhusu azma ya Tehran ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Syria kwa njia ya kisiasa na akasema Iran inaunga mkono ushiriki wowote chanya kati ya Damascus na Umoja wa Mataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 03, 2019 08:41 UTC
  • Zarif: Iran inaunga mkono ushiriki chanya wa Syria na Umoja wa Mataifa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuhusu azma ya Tehran ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Syria kwa njia ya kisiasa na akasema Iran inaunga mkono ushiriki wowote chanya kati ya Damascus na Umoja wa Mataifa.

Akizungumza leo hapa Tehran na Geir Pedersen Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Syria, Muhammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria jitihada za Tehran kwa ajili ya kutatua mgogoro wa Syria kwa njia za kisiasa na kueleza kuwa: Mashinikizo ya serikali ya Marekani yanakwamisha uundaji na kuanza kazi kamati ya katiba ya Syria. Zarif ameongeza kuwa, Iran imefanya juhudi kubwa katika mapambano dhidi ya ugaidi na vitendo vya uchupaji mipaka na kwamba Tehran siku zote inatilia mkazo kuimarishwa uhusiano kati ya Syria na Umoja wa Mataifa. 

Katika mazungumzo hayo na Zarif, Geir Pedersen Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Syria pia ameelezea hatua zilizochukuliwa hadi sasa katika mashauriano kati ya Umoja huo na baadhi ya nchi. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Syria pia wamejadili na kubadilishana mawazo kuhusu matukio ya kisiasa ya Syria na jitihada za umoja huo na nchi zinazosimamia mchakato wa Astana kuhusu kuunda na kuanza kazi kamati ya katiba ya Syria. 

Geir akiwa mazungumzoni na Zarif mjini Tehran 
 

Mazungumzo ya Astana yalianza tangu Januari mwaka 2017 kwa ubunifu wa Iran na ushirikiano wa Russia na Uturuki kwa lengo ala kurejesha amani huko Syria. Matokeo ya kwanza ya mazungumzo hayo ni kuanzishwa maeneo ya kupunguza hali ya mivutano huko Syria.