Oct 13, 2019 08:06 UTC
  • Zarif: Iran inapinga silaha za nyuklia kwa kuwa zimeharamishwa na Uislamu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inapinga vikali silaha za nyuklia kwa kuwa matumizi yake yameharamishwa na sheria za Uislamu.

Mohammad Javad Zarif amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kufafanua kuwa, "Kwa muda mrefu Kiongozi Muadhamu wa Iran amekuwa akieleza bayana kuwa, silaha za nyuklia ni haramu na matumizi yake yanakiuka mafundisho ya Uislamu. Kuziunda, kuzimiliki na kuzitumia silaha hizo ni haramu."

Dakta Zarif amebainisha kuwa, Iran inapinga vikali uundwaji na matumizi ya silaha hizo sio tu kwa kuwa zimeharamishwa na Uislamu, bali pia ni katika utekelezaji wa wajibu wake wa kijamii na kibinadamu. 

Kiongozi Muadhamu alipokutana na wanachuo wa sayansi wa Iran

Jumatano iliyopita, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alisema katu Iran haitatumia hata chembe moja ya rasilimali yake kuunda silaha za nyuklia kwa kuwa matumizi yake na kuzihifadhi kunakiuka miongozo ya Kiislamu.

Ayatullah Khamenei alisema hayo alipokutana na wanachuo wa sayansi wa Iran hapa Tehran na kusisitiza kuwa, "Sayansi ya nyuklia ina umuhimu mkubwa, lakini kwa kuwa haijaoinishwa na upendo kwa ubinadamu imebadilika kuwa maafa. Licha ya sisi kuwa na uwezo wa kuunda silaha hizo, lakini kwa ujasiri mkubwa tumejiepusha na jambo hilo kwa kuwa kuunda, kumiliki na kutumia silaha hizo ni haramu."

Tags