Jan 08, 2020 07:42 UTC
  • Watu 176 waaga dunia katika ajali ya ndege ya Ukraine mjini Tehran

Watu 176 wamepoteza maisha baada ya ndege ya abiria ya Ukraine kuanguka na kuteketea moto viungani mwa mji mkuu wa Iran, Tehran.

Reza Jafarzadeh, Msemaji wa Shirika la Usafiri wa Anga la Iran amesema aghalabu ya waliofariki dunia katika ajali hiyo ya alfajiri ya leo Jumatano katika eneo la Parand kaunti ya Robat Karim mkoani Tehran ni raia wa Iran.

Amesema abiria wote 167 na wahudumu tisa wameaga dunia katika ajali hiyo, na kwamba ndege hiyo ilikuwa ikielekea katika mji mkuu wa Ukraine, Kiev.

Ali Khashani, afisa wa ngazi za juu wa Idara ya Uhusiano Mwema katika Uwanja wa Kimataifa wa Imam Khomeini mjini Tehran amesema, ndege hiyo aina ya Boeing 737 ya Shirika la Kimataifa la Ndege la Ukraine UIA imeanguka muda mfupi baada ya kupaa angani kutoka uwanja huo, na kuteketea moto.

Ndege ya abiria ya Ukraine

Kwa mujibu wa afisa huyo, yumkini ajali hiyo imesababishwa na hitilafu za kiufundi, lakini akasisitiza kuwa, uchunguzi umeanzishwa ili kubaini kiini haswa cha ajali hiyo.

Afisa huyo wa Idara ya Uhusiano Mwema katika Uwanja wa Kimataifa wa Imam Khomeini mjini Tehran ameongeza kuwa, ajali hiyo haijatatiza ratiba na safari zingine za ndege katika angatua hiyo.

 

 

Tags