Admeri Khanzadi: Adui hana ubavu wa kuhujumu maji ya Iran
(last modified Fri, 16 Apr 2021 03:34:00 GMT )
Apr 16, 2021 03:34 UTC
  • Admeri Khanzadi: Adui hana ubavu wa kuhujumu maji ya Iran

Kamanda wa Jeshi Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema maadui hawana ubavu wala uthubutu wa kuhujumu maji ya taifa hili.

Admeri Hossein Khanzadi alisema hayo jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, maadui wa Iran wanatiwa hofu na uwezo mkubwa wa kiulinzi wa taifa hili wakifahamu fika kuwa, iwapo watajaribu kufanya kosa lolote, basi watakabiliwa kwa jibu kali la vikosi aminifu vya baharini vya Jamhuri ya Kiislamu.

Ameeleza bayana kuwa, usalama unaoshuhudiwa hivi sasa katika Ghuba ya Uajemi, Lango Bahari la Hormuz, Ghuba ya Oman na maeneo ya majini yanayopakana nayo umetokana na uwepo wa Jeshi Majini la Iran na Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC).

Kwa upande wake, Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) amesema vikosi vya majini vya Iran vitaendelea kutekeleza jukumu lake la kuhakikisha amani inakuwepo katika eneo la Ghuba ya Uajemi.

Vikosi vya majini vya Iran

 

Admeri Alireza Tangsiri amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itasimama imara kukabiliana na nchi za nje ya eneo hili na maajinabi ambao wanajiingiza kwenye Ghuba ya Uajemi kwa madhumuni ya kutoa vitisho, kuvuruga amani na kuzusha machafuko.

Amesema Jeshi Majini la Iran na Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) zitaendelea kushirikiana na kufanya kazi bega kwa bega kuanzia ngazi za chini hadi za juu.

Tags