Oct 05, 2021 08:07 UTC
  • Iran: Mazungumzo yetu na Saudia yanaendelea vizuri

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema mazungumzo baina ya Jamhuri ya Kiislamu na Saudi Arabia yanaendelea vizuri.

Akizungumza katika kikao na waandishi wa habari hapa Tehran Jumatatu juu ya mazungumzo baina ya Iran na Saudi Arabia, Saeed Khatibzadeh amesema mchakato wa mazungumzo hayo unaendelea vizuri na kwamba mazungumzo yenyewe yamejikita si tu katika mambo yanayozihusu pande mbili, lakini pia masuala ya eneo.

Amebainisha kuwa, kumekuwepo na vikao kadhaa vya mazungumzo na serikali ya Saudi Arabia huko Baghdad nchini Iraq na kuongeza kuwa, kuna maendeleo ya kuridhisha katika mazungumzo yanayohusiana na usalama wa Ghuba ya Uajemi.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza kuwa, "tunajaribu kufikia hatua ya uanzishwaji wa uhusiano endelevu uliojengeka katika fremu inayokubalika na pande mbili."

Kadhalika Khatibzadeh amepuuzilia madai ya baadhi ya vyombo vya habari kuwa ujumbe wa Saudia umeitembelea Tehran kwa ajili kufungua upya ubalozi wa Riyadh hapa nchini na kusisitiza kuwa, mazungumzo ya kisiasa na kidiplomasia baina ya Tehran na Riyadh yanafuata taratibu muafaka.

Katika hatua nyingine,  Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran ameonya kuwa, maadui hususan Marekani na Israel wanaendeleza harakati kubwa ya kupanda mbegu za chuki na mifarakano miongoni mwa mataifa ya eneo la Asia Magharibi.

Ahmad Vahidi ameyataka mataifa ya eneo yawe macho na yasimame kidete mkabala wa njama hizo za maadui; huku akiwataka maadui kujiepesha na hatua yoyote ya kichokozi dhidi ya Iran ya Kiislamu.

 

Tags