Kuanza safari ya Rais wa Uturuki mjini Tehran
Rais Tayyip Erdoğan wa Uturuki Recep ataswasili hapa mjini Tehran leo Jumatatu jioni (Julai 18) akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa maafisa wa kisiasa na kiuchumi wa nchi yake ikiwa ni katika kujibu mwaliko rasmi wa Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika safari hii ya Rais wa Uturuki na ujumbe anaoandamana nao, maafisa wa pande mbili watapitia mchakato unaokuwa wa ushirikiano wa kiuchumi, kibiashara na kisiasa kati ya nchi hizi. Mbali na mikutano hiyo, madhumuni mengine ya ziara ya Rais wa Uturuki mjini Tehran ni kushiriki katika mkutano wa saba wa wakuu wa nchi ambazo ni wadhamini wa mchakato wa Astana, utakaofanyika mjini Tehran kwa ushiriki wa marais wa Iran, Russia na Uturuki.
Kuhusiana na hilo, imepangwa kuwa sherehe rasmi ya kumkaribisha rais wa Uturuki itafanyika Jumanne asubuhi (Julai 19) katika jumba la kihistoria na kiutamaduni la Saadabad, mjini Tehran. Ziara ya Erdoğan mjini Tehran inafanyika huku Rais Vladimir Putin wa Russia pia akitazamiwa kuwasili Tehran na kujiunga na mkutano wa kilele wa nchi hizi tatu. Wakati wa kufanyika mkutano wa saba wa viongozi wa Iran, Russia na Uturuki, masuala yanayohusiana na mzozo wa ndani wa Syria yatajadiliwa. Kwa msingi huo, mkutano wa Tehran ni muhimu kwa nchi tatu zinazoshiriki na pia kwa serikali na mataifa mengine ya eneo na dunia kwa ujumla.
Kuchunguzwa uhusiano wa Iran na Uturuki kama nchi mbili jirani na za Kiislamu ni muhimu katika mitazamo miwili ya kikanda na kimataifa. Na hasa ikitiliwa maanani kuwa katika miaka ya hivi karibuni, nchi mbili zimethibitisha kivitendo kwamba zina uwezo wa kuwa na nafasi athirifu kwa nchi zingine katika eneo na hata katika upeo wa kimataifa. Katika uwanja wa mahusiano ya kiuchumi kati ya Iran na Uturuki, inatupasa tuseme kuwa uhusiano kati ya nchi hizi mbili unazidi kuimarika kila siku. Suala hilo linaonyesha kuwa Tehran na Ankara zimedhamiria kuimarisha ushirikiano wa pande mbili.
Katika upande wa ushirikiano wa kieneo, ushiriki wa Iran na Uturuki katika mchakato wa kutatua matatizo ya ndani ya Syria unathibitisha ukweli kwamba, tawala za kibeberu za Magharibi zilizokuwa zikiamua hatima ya nchi za Asia Magharibi, sasa zinapasa kufunga virago na kurudi katika mabara yao. Iran na Uturuki pamoja na Russia zinaweza kutatua matatizo ya kanda hii na kumaliza mizozo yake ya ndani, ikiwemo ya Syria bila kuhitajia uingiliaji wa nchi za Magharibi. Ingawa kuna changamoto katika uwanja huo, lakini inatarajiwa kwamba changamoto hizo zitapungua na kumalizika hivi karibuni. Hakuna shaka kuwa uwepo wa washauri wa Iran na Russia nchini Syria ni jambo linalofanyika kwa idhini ya serikali halali ya Rais Bashar al-Assad wa nchi hiyo.
Hii ni katika hali ambayo uwepo wa jeshi la Uturuki katika nchi hiyo ya Kiarabu umefanywa kinyume cha sheria na hivi karibuni jeshi hilo litalazimika kuondoka Syria na kurejea nchini kwake. Tangu mwaka 2011, serikali ya Uturuki iliunga mkono kupinduliwa kwa serikali halali ya Bashar al-Assad nchini Syria, ikishirikiana na serikali za Magharibi zinazoongozwa na Marekani na baadhi ya serikali za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi. Mnamo 2018, serikali ya Uturuki ilivamia Syria na kukalia kwa mabavu sehemu ya ardhi yake kutokana na hitilafu zilizojitokeza baina yake na Marekani. Ni dhahiri kwamba hatua hiyo ya jeshi la Uturuki ilifanyika kinyume cha sheria za kimataifa. Baadhi ya wataalamu wanadhani kwamba hatua hiyo ilichukuliwa katika fremu ya mfumo mpya wa dunia ambao unadhamiria kuiondoa dunia katika mfumo wa kambi moja inayoongozwa na Marekani na kuielekeza katika mfumo wa kambi kadhaa za udhibiti na satua ya kiutawala.
Kuhusiana na hilo, "Harut Artin Araklian", mtaalamu mashuhuri wa Armenia katika masuala ya kimataifa anasema: "Katika mfumo mpya wa dunia unaozaliwa hivi leo, Uturuki inajaribu kuchukua nafasi ya nguvu ya tatu. Iwapo haitafanikiwa kufikia lengo hilo, itaondoka uwanjani. Leo Uturuki ni mchokozi nchini Syria."
Wakati huo huo, mtaalamu huyu wa Kiarmenia anasema:
"Uturuki inaelekea upande wa Ulaya kwa kujaribu kunyonya rasilimali zote za mafuta na gesi za Syria, Azerbaijan na Turkmenistan. Hizi ndizo zana ambazo Ankara itacheza nazo katika siku zijazo, na ikiwa haitapata fursa ya kufanya hivyo basi itasukumwa "pembeni".
Hata hivyo, ziara ya Rais wa Jamhuri ya Uturuki na ujumbe wake wa ngazi za juu mjini Tehran ni muhimu sana kwa ushirikiano wa pande mbili. Kwa sababu katika safari hii, sehemu muhimu ya ushirikiano kati ya Iran na Uturuki itatayarishwa kwa ahili ya mwaka ujao. Wakati huo huo kufanyika mkutano wa saba wa viongozi wa Iran, Russia na Uturuki mjini Tehran ni fursa nyingine kwa ajili ya nchi hizo tatu kupanga mikakati ya kuhitimisha matatizo ya ndani na kieneo ya Syria. Iwapo maazimio ya mkutano wa Tehran yatatekelezwa, bila shaka, Marekani ambayo inaiba mafuta ya Syria, italazimika kuondoka nchini humo na kurejea Washington.