Azma ya Iran ya kukabiliana na magaidi wanaotaka kujitenga kaskazini mwa Iraq
Vikosi vya makombora na ndege zisizo na rubani za Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mara nyingine tena vimelenga makao makuu ya makundi ya kigaidi ya Komoleh na Democratic katika mikoa ya Sulaymaniyah na Erbil nchini Iraq.
Mashambulizi dhidi ya magaidi wanaotaka kujitenga nchini Iran yamefanywa katika hali ambayo Iran imetahadharisha katika siku za karibuni kwamba iwapo serikali ya Iraq haitochukua hatua dhidi ya makundi hayo, basi Iran haitakuwa na budi ila kuendeleza mashambulizi dhidi ya makundi hayo katika eneo la Kurdistan nchini Iraq. Kwa hivyo, mashambulizi yaliyofanywa jana asubuhi yanaonyesha wazi azma thabiti iliyonayo Iran katika kukabiliana na vitisho vya kiusalama na kijeshi vilivyo karibu na mipaka yake.
Kwa maneno mengine ni kwamba mashambulizi ambayo yamekuwa yakifanywa na Iran katika wiki za hivi karibuni yanaonyesha wazi kuwa subira iliyokuwanayo Iran kuhusiana na vitisho hivyo imefikia tamati. Mashambulizi hayo ya jana asubuhi hayakuwa na mfano wake katika mtazamo wa wingi na ubora kwa sababu mkoa wa Sulaymaniyah kwenye mpaka wa Iran na maeneo tofauti ya Erbil, yote hayo yalishambuliwa kwa makombora na ndege zisizo na rubani.
Suala jengine ni kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafahamu vyema kuwa makundi hayo ya kigaidi yanaungwa mkono na utawala wa Kizayuni na baadhi ya nchi za kibeberu ikiwemo Marekani. Kwa upande mwingine, nyayo za makundi hayo pia zinaonekana wazi katika machafuko ya hivi karibuni nchini Iran. Magaidi hao wanaotaka kujitenga, kwa kujipenyeza ndani ya ardhi ya Iran na kuchanganyika na watu wa kawaida na baadhi ya raia wanaoandamana, wanazua fujo na pia kutekeleza mradi wa mauaji dhidi ya watu wasio na hatia pamoja na kuharibu mali za umma. Kwa ajili hiyo Iran imechukua tahadhari zaidi na inaendelea kuyashambulia makundi ya kigaidi kaskazini mwa Iraq licha ya mashinikizo ya kisaikolojia ya Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi dhidi yake.
Nukta ya tatu ni kwamba inaonekana kuwa, mashambulizi dhidi ya magaidi wanaotaka kujitenga huko kaskazini mwa Iraq huenda yanatekelezwa kwa ushirikiano au kwa uchache kwa ufahamu wa serikali kuu ya Baghdad. Hivi karibuni, Brigedia Jenerali Esmail Qaani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu alikutana na kuzungumza na viongozi wa Iraq mjini Baghdad, ambapo pia Fuad Hossein na Hossein Amirabdollahian, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iraq na Iran kwa utaratibu huo walikutana na kujadiliana kuhusu masuala tofauti yanayozihusu pande mbili hizo.
Katika mazungumzo hayo, viongozi wa Iraq walifahamishwa kutoridhishwa Iran na suala zima la usalama katika mipaka yake ya Magharibi na hasa uwepo katika ardhi ya Iraq magaidi wanaotaka kujitenga na vilevile maafisa wa kijasusi na usalama wa Kizayuni huko kaskazini mwa Iraq.
Kisheria na kwa kuzingatia kifungu cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa, Iran ina haki ya kuendesha operesheni za kijeshi dhidi ya magaidi wenye silaha wanaotaka kujitenga, wanaofanya mauaji na kuvuruga usalama wake. Khusiana na hilo, kifungu cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa kinasema: Iwapo mwanachama wa Umoja wa Mataifa atakabiliwa na uvamizi wa kutumia silaha, hakuna kipengee chochocte cha hati hii kitakachozuia haki ya asili ya mtu binafsi au jamii kujitetea hadi pale Baraza la Usalama litakapochukua hatua zinazohitajika ili kudumisha amani na usalama kimataifa.
Katika kujibu mashambulizi ya Iran dhidi ya magaidi walioweka kambi zao za kijeshi kaskazini mwa Iraq, Wamarekani wamedai kuwa mashambulizi hayo yanakiuka uhuru wa kujitawala Iraq. Kwa kutilia maanani kwamba Iran imeifahamisha mapema serikali ya Baghdad kuhusu mashambulizi dhidi ya magaidi na pia Kifungu cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa kinaipa haki ya kujitetea na kujilinda dhidi ya magaidi, madai ya Wamarekani kuhusu ukiukaji wa Iran wa kujitawala Iraq ni batili na bila shaka yanalenga kuibua fitina na mgawanyiko kati ya nchi mbili hizi jirani.