Sisitizo la Kiongozi Muadhamu la umuhimu wa kimkakati wa sekta ya nyuklia
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, sekta ya nyuklia ya Iran ni ufunguo wa maendeleo na ustawi wa nchi katika nyuga mbalimbali.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alisema hayo Jumapili ya jana tarehe 11 Juni alipoonana na wanasayansi, wataalamu na wabobezi wa masuala ya nyuklia wa Iran. Ayatullah Khamenei ameashiria taathira za kimsingi za mafanikio ya nyuklia katika kuboresha maisha ya wananchi wa Iran na kuongeza kuwa, sekta ya nyuklia kwa upande wa uzito wa kisiasa na nafasi ya taifa kimataifa inapelekea kupatikana heshima ya kitaifa na wakati huo huo kinyume na juhudi za maadui za kuifanya nchi ionekane ya kukosa matumaini na kuwakatisha tamaa vijana, inafufua ari, moyo wa matumaini na hali ya kujiamini kwa taifa katika jamii na kuwaonyesha wananchi hasa vijana kuwa inawezekana kuingia katika medani kubwa na kuwa na nafasi muhimu.
Kadhalika Ayatullah Khamenei amesema, kila ambaye anaipenda Iran, Jamhuri ya Kiislamu, nguvu na maendeleo ya taifa hili, anapaswa kuzipa umuhimu harakati za kielimu, utafiti na sekta ya nyuklia. Vilevile amesema, kufanywa teknolojia ya nyuklia kuwa ya ndani ya Iran ni jambo muhimu sana na ni pigo kwa Magharibi na kwa watu wenye fikra za Kimagharibi ambao wanafanya njama za kulidhalilisha taifa na kudhoofisha moyo wa kufanya kazi na kuishi kwa matumaini mazuri.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amesema, maadui hawataki kabisa kuona taifa la Iran linapiga hatua za maendeleo na ndiyo sababu kuu inayowafanya waisakame sana Iran katika kadhia yake ya nyuklia.
Kama ambavyo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha mara chungu nzima, hii leo ulazima wa kupatikana teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani kwa ajili ya kudhamini usalama na maendeleo ya nchi ni suala lisilopingika; teknolojia ya nyuklia ni moja ya teknolojia mhimili na ya kimsingi ambayo ina mchango mkubwa katika maendeleo ya teknolojia mpya na maendeleo ya viwanda vipya. Filihali, teknolojia ya nyuklia nchini Iran inatumika katika sekta mbalimbali kama vile tiba, nishati, uzalishaji wa dawa, kilimo, bidhaa za viwandani na za kiteknolojia. Hili si tu kwamba limezuia fedha za kigeni kutoka nchini, bali limepelekea pia bidhaa nyingi ambazo hapo awali zilikuwa zilikihodhiwa tu na madola ya Magharibi, kuzalishwa pia hapa nchini Iran na hivyo kuvunja ukuta wa maradhi ya ukiritimba wa madola ya Magharibi ya kutaka kuhodhi kila kitu.
Fauka ya hayo, baadhi ya miradi imeondoka katika hatua ya kiutafiti katika vituo vya kiutafiti na kufikia kiwango cha kiviwanda na uzalishaji. Hivi sasa wanasayansi wa Iran wamepata maendeleo makubwa katika uga wa dawa za mionzi (radiopharmaceuticals). Hii ni katika hali ambayo, karibu 90% ya vifaa katika uwanja wa teknolojia ya nyuklia vinazalishwa hapa nchini na bila shaka haya ni matunda ya hima, idili na uchapakazi kazi wa wanasayansi wa Iran.
Kutokana na kuongezeka kila leo matumizi ya sekta ya nyuklia, sekta hii inavutia hisia za nchi nyingi, na Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran pia lina majukumu kadhaa ya kipaumbele linayoyafuatilia, ikiwa ni pamoja na uwanja wa mzunguko wa fueli ya nyuklia, uga wa uzalishaji wa umeme na vinu vya nyuklia, na mambo mengine ambayo hutumiwa katika sekta ya afya, mazingira, kilimo na bidhaa za chakula.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, katika miaka ya hivi karibuni, maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakiwa na lengo la kuzuia maendeleo ya nyuklia ya Iran ambayo inahesabiwa kuwa ni sehemu ya nguvu ya nchi, mbali na kutekeleza mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi, hata kuwaua wanasayansi wa Iran na kuwafanyia hujuma, wamefanya uharibifu pia katika vituo vya nyuklia vya Iran. Hata hivyo ustawi na maendeleo ya Iran katika nyanja mbalimbali, ikiwemo sekta ya nyuklia, yamethibitisha kwamba, njama za maadui za kusambaratisha vielelezo vya nguvu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimeshindwa na kugonga ukuta.