Kukamilika mchakato wa uanachama wa Iran katika Jumuiya ya Shanghai
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i99442-kukamilika_mchakato_wa_uanachama_wa_iran_katika_jumuiya_ya_shanghai
Uanachama rasmi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai unatarajiwa kukamilika katika kikao kijacho cha jumuiya hiyo tarehe 4 Julai.
(last modified 2026-05-10T14:24:40+00:00 )
Jul 02, 2023 07:50 UTC
  • Kukamilika mchakato wa uanachama wa Iran katika Jumuiya ya Shanghai

Uanachama rasmi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai unatarajiwa kukamilika katika kikao kijacho cha jumuiya hiyo tarehe 4 Julai.

Katika mazungumzi yake kwa njia ya simu na Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Zhang Ming, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) sambamba na kufurahishwa kwake na Iran kuwa mwanachama kamili katika jumuiya hiyo amesisitiza kuwa, uanchama kamili katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai utatangazwa rasmi katika mkutano ujao na kuanzia Julai nne siku ya Jumanne, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itakuwa na haki zote ambazo ni makhsusi kwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

Wiki iliyopita pia, Bakhtiyar Hakimov, mjumbe wa Rais wa Russia katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai alisema kuwa, Iran imekamilisha hatua zote za lazima kwa ajili ya kuwa mwanachama kamili wa jumuiya hiyo na katika mkutano ujao ambao utafanyika mjini New Delhi, India kwa njia ya mawasiliano ya intaneti, Iran itakubaliwa rasmi kama mwanachama kamili. Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai iliyoanzishwa mwaka wa 2001 ni muungano baina ya mabara uliojikita katika ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kiusalama.

Jumuiya hii sambamba na kuwa na karibu asilimia 40 ya idadi ya watu duniani, inajumuisha asilimia 28 ya pato ghafi la dunia. Hii leo uanachama katika mashirika kama vile Shanghai, ambayo pamoja na mafanikio makubwa ya kiuchumi, pia yana mwelekeo wake maalumu wa kisiasa na usalama, ni jambo muhimu sana kwa mataifa mbalimbali, kwa sababu uanachama katika mashirika ya kimataifa huongeza uwezo wa kiuchumi wa nchi na pia huongeza ushirikiano wa pande kadhaa wa kimataifa.

 

Kwa kutilia maanani kwamba, maingiliano na mafungamano na nchi za eneo zikiwemo nchi wanachama wa Jumuiya ya Shanghai na kuwepo kwa ufanisi katika mipango ya kieneo na kimataifa ni kiini cha siasa za nje za serikali ya awamu ya 13 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ndio maana katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, serikali ya Iran imekuwa ikifanya kazi ya kuboresha uhusiano na nchi wanachama katika jumuiya hii na imepata mwafaka wa wanachama wote wa Shanghai. Katika muktadha huu, Septemba 2021, Rais Sayyid Ibrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alifanya safari nchini Tajikistan na kushiriki katika mkutano wa 21 wa wakuu wa Jumuiya ya Shanghai na kuweza kubadilisha uanachama wa Iran katika jumuiya hiyo kutoka mwanachama mtazamaji na kuwa mwanachama wa kudumu.

Hapana shaka kwamba, kuwa Iran mwaanachama kamili wa jumuiya ya shanghai kuna umuhimu kwa pande mbalimbali za kisiasa na kiuchumi. Hii ni kutokana na kuwa, baada ya hapa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa mmoja wa wanachama wa kudumu na wakuu wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai itakuwa na anga mwafaka zaidi kwa ajili ya ushirikiano wa kimataifa katika nyuga za kisiasa, kiusalama, kiuchumi, kimasoko, kifedha na kibenki. Hii ni katika hali ambayo, Iran inaandamwa na vikwazo haramu na vya upande mmoja vya Marekani na kwa msingi huo, uanachama kamili katika Shanghai mbali na kuipatia Iran faida za kiuchumi, hilo linahesabiwa kuwa pigo kubwa kwa Marekani na sera za nchi hiyo zenye lengo la kuitenga Tehran.

Inapasa kuzingatia kwamba, nafasi ya kijiopolitiki na vyanzo vya mafuta na gesi vya Iran ni jambo lenye umuhimu sana kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Shanghai.

 

Iran ni miongoni mwa nchi chache duniani ambazo ziko katika maeneo kadhaa ya muhimu. Ukweli wa mambo ni kuwa, Iran iko katika eneo la Ghuba ya Uajemi, Asia ya Magharibi, Asia ya Kati, Caucasus na Bara Hindi, na hivyo kuwa katika eneo maalumu na nyeti. Iran inahesabiwa kuwa ni daraja kati ya bara la Asia, Ulaya na Afrika. Pia, uanachama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama mojawapo ya wamiliki wakubwa wa rasilimali za mafuta na gesi unachukuliwa kuwa ni muhimu kwa wanachama wa Shanghai ikiwa ni pamoja na China ikiwa mtumiaji mkubwa zaidi wa nishati.

Kwa hivyo, kuweko Iran katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai kutaongeza umuhimu na nafasi ya jumuiya hii katika uhusiano wa kimataifa. Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran sambamba na kuashiria suala hili katika mazungumzo yake ya simu na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai amesema, nina imani kuwa, kukubaliwa rasmi uanachama wa Iran katika Jumuiya ya Shangahi, kutatoa uwezo mpya na utaongezeka nguvu na uwezo mpya kwa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai.