UNICEF yaonya kuhusu hali mbaya ya Gaza kwa watoto
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i106098-unicef_yaonya_kuhusu_hali_mbaya_ya_gaza_kwa_watoto
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limetangaza kuwa, kufuatia mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza, Ukanda huo umekuwa sehemu hatari zaidi duniani kwa watoto.
(last modified 2023-12-17T04:27:02+00:00 )
Dec 17, 2023 04:27 UTC
  • UNICEF yaonya kuhusu hali mbaya ya Gaza kwa watoto

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limetangaza kuwa, kufuatia mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza, Ukanda huo umekuwa sehemu hatari zaidi duniani kwa watoto.

Ripoti ya UNICEF kuhusu hali ya Gaza inaonyesha kwamba takriban watoto milioni moja huko Gaza wamefurushwa kwa nguvu kutoka makwao.

Msemaji wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef) ameripoti kuhusu kuuliwa idadi kubwa ya watoto huko Ukanda wa Gaza.

James Elder amenukuliwa akisema kuwa, ameshuhudia kwa macho yake mwenyewe watoto wa Kipalestina walioungua sana, waliodhurika ubongo na mifupa yao kuvunjika  kutokana na mashambulizi ya Israel. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) linaeleza kwamba, maelfu ya watoto wa Kipalestina wanahitaji misaada ya kibinadamu huku wakiendelea kuteseka na matokeo mabaya ya vita vya kikatili vya Isreal katika eneo hilo.

 

Takwimu zilizoripotiwa na shirika la misaada la Save the Children zinaonyesha idadi ya watoto waliouawa katika Ukanda wa Gaza kutokana na uvamizi unaoendelea wa Israel imepita takwimu za kila mwaka zinazohusiana na migogoro ya kimataifa katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Wakati huo huo, Carl Skau, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Dunia (WFP) ameeleza kuwa, hali ya kibinadamu ya Uganda wa Gaza ni mbaya mno. Afisa huyo  wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa, asilimia 50 ya wakazi wa eneo la Palestina la Ukanda wa Gaza linalokaliwa kwa mabavu wapo hatari ya kupoteza maisha kutokana na makali ya njaa.