Israel yaua mwanadiplomasia wa Ufaransa Ukanda wa Gaza, Paris yataka maelezo
Shirika la Habari la Ujerumani limeinukuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa ikisema kuwa mwanadiplomasia wa nchi hiyo amefariki dunia kutokana na majeraha aliyoyapata wakati wa mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza.
Taarifa iliyotolewa na Wizara Mambo ya Nje ya Ufaransa imesema kwamba afisa huyo pamoja na wenzake wawili na wanafamilia alikuwa amekimbilia katika nyumba ya mmoja wa wafanyakazi wenzake katika ubalozi mdogo wa Ufaransa huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza, karibu na mpaka na Misri wakati waliposhambuliwa na jeshi al Israel.
Taarifa hiyo imesema kuwa nyumba hiyo ilishambuliwa na Israel Jumatano iliyopita, na kusababisha mwanadiplomasia huyo kujeruhiwa na kuua watu wengine 10.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa imeongeza kuwa, mwanadiplomasia huyo - ambaye alikuwa akifanya kazi na serikali ya Ufaransa tangu 2002 – aliaga dunia baadaye kutokana na majeraha, na kwamba "Ufaransa inalaani shambulio la bomu la Israel lililolenga jengo la makazi ambalo lilisababisha vifo vya raia wengine wengi."

Ufaransa imeitaka Israel "kutoa ufafanuzi kamili kuhusu mazingira ya shambulio hilo haraka iwezekanavyo."
Israel ilianzisha vita dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza mapema mwezi Oktoba mwaka huu na hadi sasa imeua shahidi karibu watu 20,000 - wengi wao wakiwa watoto na wanawake. Makumi ya maelfu na wengine wamejeruhiwa, na Wapalestina zaidi ya milioni moja wamelazimika kuwa wakimbizi baada ya makazi na nyumba zao kuharibiwa kwa mashambulizi ya pande zote ya jeshi katili la Israel.