Wazayuni waomba mazungumzo, muqawama washurutisha kukomeshwa vita kwanza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i106122-wazayuni_waomba_mazungumzo_muqawama_washurutisha_kukomeshwa_vita_kwanza
Mkuu wa shirika la kijasusi la Israel MOSSAD amesema kuwa, viongozi wa kisiasa wa utawala wa Kizayuni wamempa idhini ya kufanya mazungumzo kuhusu kusimamishwa vita kwa muda na kwa ajili ya kubadilishana mateka, lakini viongozi wa HAMAS wamesema kuwa, hawakubali kufanya mazungumzo yoyote mpaka kwanza vita visimamishwe kikamilifu.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Dec 18, 2023 03:42 UTC
  • Wazayuni waomba mazungumzo, muqawama washurutisha kukomeshwa vita kwanza

Mkuu wa shirika la kijasusi la Israel MOSSAD amesema kuwa, viongozi wa kisiasa wa utawala wa Kizayuni wamempa idhini ya kufanya mazungumzo kuhusu kusimamishwa vita kwa muda na kwa ajili ya kubadilishana mateka, lakini viongozi wa HAMAS wamesema kuwa, hawakubali kufanya mazungumzo yoyote mpaka kwanza vita visimamishwe kikamilifu.

Shirika la habari la Mehr limeinukuu kanali ya 12 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni ikitangaza kuwa, mkuu wa Mossad, David Barnea amepewa idhini na wakuu wa kisiasa wa Israel kuendelea na mazungumzo ya kubadilishana mateka kwa upatanishi wa baadhi ya nchi.

Kwa upande wake, tovuti ya habari ya Axios ya nchini Marekani imenukuu maafisa wa kuaminika na kusema kuwa, mwishoni mwa wiki hii, mkuu wa Mossad ataonana tena na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar kwa ajili ya kuendeleza juhudi za kuanzisha tena mazungumzo ya kubadilishana mateka. 

Hivi karibuni utawala wa Kizayuni wa Israel uliwaua mateka wake watatu na kudai kuwa imefanya mauaji hayo kimakosa.

Wanamapambano wa HAMAS

 

Kwa upande wake, viongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS wamekuwa wakisisititizia msimamo wao kuwa hakuna mazungumzo yoyote mengine yatakayofanyika ila baada ya utawala wa Kizayuni kukomesha kikamilifu mashambulizi yake ya kikatili dhidi ya raia wa Ghaza.

Usama Hamdan, mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa HAMAS kabla ya hapo alikuwa amenukuliwa akisema kuwa, sharti la kuanza mazungumzo yoyote mengine ni kukomeshwa mashambulizi ya Israel dhidi ya wanananchi wa Ghaza.

Baada ya kupita zaidi ya miezi miwili ya kufanya jinai za kutisha kwa madai ya kuangamiza makundi ya muqawama ya Palestina ikiwemo HAMAS na kukomboa mateka Wazayuni, hadi hivi sasa utawala wa Kizayuni umeshindwa kufikia hata lengo moja ulilodai kulifuatilia kwenye jinai zake hizo.