Hamas: Hakuna mazungumzo ya kubadilishana mateka kabla ya Israel kusimamisha vita
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i106132-hamas_hakuna_mazungumzo_ya_kubadilishana_mateka_kabla_ya_israel_kusimamisha_vita
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, haitajihusisha na majadiliano yoyote kuhusu kubadilishana wafungwa kwa mateka kabla ya utawala ghasibu wa Israel kusimamisha kabisa mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2026-07-03T11:45:53+00:00 )
Dec 18, 2023 03:17 UTC
  • Hamas: Hakuna mazungumzo ya kubadilishana mateka kabla ya Israel kusimamisha vita

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, haitajihusisha na majadiliano yoyote kuhusu kubadilishana wafungwa kwa mateka kabla ya utawala ghasibu wa Israel kusimamisha kabisa mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza.

Katika ujumbe siku ya Jumapili, harakati hiyo ya Kiislamu imesema "imewasilisha msimamo huo kwa wapatanishi wote."

Israel ilianzisha vita vya kikatili huko Gaza tarehe 7 Oktoba baada ya Hamas kutekeleza Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa ili kulipiza kisasi kwa ukatili wa Israel dhidi ya watu wa Palestina.

Tangu kuanza mashambulizi hayo, utawala wa Tel Aviv umeua Wapalestina zaidi ya 20,000 wengi wao wakiwa wanawake na watoto na kuwajeruhi wengine 54,450.

Kama sehemu ya usitishaji vita wa wiki moja wa kibinadamu, uliosimamiwa na Qatar na Misri, mapigano yalisitishwa na misaada ya kibinadamu iliruhusiwa kuingia Gaza kwa muda, ambayo iko chini ya mzingiro kamili wa Israel.

Gaza

Pia ilishuhudia mabadilishano kati ya wafungwa wa Kipalestina 240 wanaoshikiliwa na Israel na mateka 105 wa vita, wakiwemo Waisraeli 81 na wageni 24, huko Gaza.

Israel inaamini kuwa takriban wafungwa 137 bado wanazuiliwa huko Gaza, huku ikifikiriwa kuwa kuna Wapalestina 7,000 katika magereza ya Israel, wengi wao wakizuiliwa bila kufunguliwa mashtaka.