Ismail Haniya: Muqawama wa Wapalestina ni imara
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i106244-ismail_haniya_muqawama_wa_wapalestina_ni_imara
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu (Muqawama) ya Palestina, Hamas, Ismail Haniya amesisitiza uthabiti na azma ya harakati hiyo katika kuendeleza mapambano ya kupigania ukombozi wa Palestina.
(last modified 2023-12-21T03:11:01+00:00 )
Dec 21, 2023 03:11 UTC
  • Ismail Haniya: Muqawama wa Wapalestina ni imara

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu (Muqawama) ya Palestina, Hamas, Ismail Haniya amesisitiza uthabiti na azma ya harakati hiyo katika kuendeleza mapambano ya kupigania ukombozi wa Palestina.

Akizungumza Jumatano katika kikao na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir Abdollahian mjini Doha, Qatar, Haniya ameeleza mashambulizi ya utawala wa Israel katika Ukanda wa Gaza kutoka nchi kavu, angani na baharini kuwa hayajawahi kushuhudiwa lakini akasisitiza kuwa wameshindwa kuiangusha harakati ya Hamas.

'Baada ya siku 75 za ukatili na jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni huko Gaza, muqawama umeendelea kuwa imara na wenye nguvu na umesababisha hasara kubwa kwa adui,' amesema.

Amesema maelfu ya watu wengi wao wakiwa wanawake na watoto wameuawa shahidi au kujeruhiwa na maelfu ya nyumba na majengo yameharibiwa katika mashambulizi ya Israel lakini wananchi wa Palestina wanaendelea na njia ya muqawama ili kuushinda utawala wa Kizayuni.

Katika kikao chao, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na kiongozi huyo wa Hamas wamebadilishana mawazo kuhusu matukio ya hivi punde huko Palestina, hususan katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Amir-Abdollahian kwa upande wake amesisitiza kuwa Iran itaendelea na juhudi zake za kidiplomasia za kuunga mkono "taifa la Palestina linalodhulumiwa lakini lenye nguvu na subira." Amesema uungaji mkono huo unalenga kukomesha vita, jinai na mzingiro wa Israel dhidi ya Gaza na kukabiliana na njama za kisiasa zinazoupa himaya utawala dhalimu wa Israel.

"Leo hii, hakuna mwenye shaka kuwa taifa la Palestina kwa mapambano na muqawama limethibitisha nguvu na azma mbele ya njama ya mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni licha ya kustahimili maumivu na mateso mengi na kuwatoa mhanga zaidi ya mashahidi 20,000 katika siku 75 zilizopita."

Hali baada ya hujuma ya Israel katika eneo la raia Gaza

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amelaani uungaji mkono wa Marekani "wa pande zote na usio na kikomo" kwa Israel katika vita vya Gaza, akiitaka Washington kuacha uungaji mkono wake usio na tija wa "mkakati wa kijeshi wa kichaa" wa Tel Aviv.

Wakati huo huo, Haniya alielekea Cairo, Misri jana Jumatano kwa ajili ya mazungumzo ya kusitisha mapigano huko Gaza.

Bado hakuna maelezo zaidi kuhusu safari hiyo lakini harakati ya muqawama wa Palestina tayari imefutilia mbali mabadilishano ya wafungwa na utawala wa Kizayuni maadamu vita vinaendelea.

Utawala wa Kizayuni umekuwa ukiendesha vita vya kikatili katika Ukanda wa Ghaza tokea tarehe 7 Oktoba, vita ambavyo kwa mujibu wa maafisa wa Palestina na duru za Umoja wa Mataifa, mbali na kusababisha maafa ya kibinadamu ambayo hayajawahi kushuhudiwa, vimeharibu miundombinu mingi na kuua shahidi maelfu ya raia, wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake.