Afisa wa Yemeni: Marekani ikifanya ujinga, jeshi letu litapigana nayo
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i106268-afisa_wa_yemeni_marekani_ikifanya_ujinga_jeshi_letu_litapigana_nayo
Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema iwapo Marekani inataka kufanya ujinga mpya, jeshi la Yemen litakuwa tayari kukabiliana nayo na lina chaguzi za kushangaza.
(last modified 2023-12-21T23:35:40+00:00 )
Dec 21, 2023 23:35 UTC
  • Afisa wa Yemeni: Marekani ikifanya ujinga, jeshi letu litapigana nayo

Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema iwapo Marekani inataka kufanya ujinga mpya, jeshi la Yemen litakuwa tayari kukabiliana nayo na lina chaguzi za kushangaza.

Hazzam Mohammad Al-Assad ameliambia Shirika la Habari la Iran (IRNA) kwamba: "Hatushangazwi na msimamo wa hivi karibuni wa Marekani na tangazo la kuundwa muungano wa kijeshi wa kulinda meli za utawala wa Israel zinazoelekea kwenye bandari za utawala huo, kwa sababu tangu mwanzo, Washington ndiyo inayosimamia na kuendesha mashambulizi dhidi ya watu wa Gaza na imekuwa ikifanya jitihada za kuzuia makombora na ndege zisizo na rubani za Yemen zisimfikie adui wa Mzayuni."

Mohammad Al-Assad amesema, nafasi ya Marekani katika kuuhami utawala wa Kizayuni wa Israel haifichiki kwa mtu yeyote, na tangu dakika ya kwanza kabisa ya operesheni ya "Kimbunga cha Al Aqsa, Washington iliuunga mkono na kuusaidia utawala huo ghasibu katika ngazi mbalimbali hasa ngazi ya kijeshi, na inaupatia silaha kwa ajili ya kuua wanawake na watoto wa Palestina.

Hizzam al-Assad ameongeza kuwa, uamuzi wa Abdul Malik Badruddin al-Houthi, kiongozi wa harakati ya Ansarullah, wa kuwaunga mkono kikamilifu ndugu zake wa Gaza, ni msimamo unaozingatia maadili yetu ya kidini, kibinaadamu na kiakhlaki na ulichukuliwa kujibu ombi la msaada kutoka kwa watu wa Gaza na matakwa ya taifa azizi la Yemen.

Mjumbe huyo wa Ansarullah ya Yemen amesema, muungano wa baharini wa Marekani ulizaliwa ukiwa umekufa na kuundwa kwake hakuna msingi wala marejeo yoyote, bali lengo lake pekee ni kulinda meli za utawala wa katili wa Israel, huku zaidi ya watu milioni mbili huko Gaza wakiendelea kupigwa kwa mabomu na kuuawa.

Israel inaendelea kuua watoto wa Gaza kwa msaada wa Marekani na washirika wake.

Katika kuwaunga mkono watu wa Palestina, Jeshi la Wanamaji la Yemen limepiga marufuku kupita meli zote za Israel zinazoelekea Palestina inayokaliwa kwa mabavu katika lango bahari la Bab al-Mandab, na mbali na kukamata meli ya Israel iitwayo "Galaxy Leader", limeshambulia meli kadhaa za Israel na zisizo za Israel zilizokuwa njiani kuelekea Israel ambayo zimepuuza maonyo Jeshi la Yemen.