Askari 11 wa kikosi maalumu cha Israel waangamizwa kaskazini mwa Gaza
Mapigano kati ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel na Brigedi za Al Qassam kaskazini mwa Ukanda wa Gaza yamepelekea kuangamizwa wanajeshi kadhaa wa kikosi maalumu cha utawala huo.
Shirika la habari la Shihab limeripoti kuwa, Brigedi za Izzuddin Al Qassam tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) zimepigana na kundi moja la makomando wa utawala wa Kizayuni katika eneo la al Toam kaskazini mwa mji wa Gaza; ambapo wanajeshi 11 wa kikosi maalumu cha Israel wameangamizwa.
Wanamapambano wa Al Qassam pia wamelishambulia kundi moja la wanajeshi wa Israel huko kaskazini mwa Gaza. Wanamapambano wa al Qassam wamekabiliana na wanajeshi wa Kizayuni na kufanikiwa kuangamiza na kujeruhi wanajeshi kadhaa wa utawala huo ghasibu.
Jeshi la Israel limetangaza kuwa idadi ya wanajeshi wake waliouawa hadi sasa tangu kuanza vita dhidi ya Gaza kuwa ni 469. Hata hivyo vyombo vya kujitegemea vinasema idadi halisi ya askari wa Israel waliouawa katika vita vya Gaza ni kubwa zaidi kuliko ile inayotajwa na Israel.