Umoja wa Mataifa wataka misaada zaidi Gaza baada ya kupasiswa azimio
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa mwito wa kuongezwa misaada zaidi ya kibinadamu kwa watu wa Gaza wanaokabiliwa na hali mbaya ya uhaba wa chakula na huduma zingine muhimu.
Hii ni baada ya Baraza la Usalama hatimaye kulipigia kura azimio kuhusu Gaza baada ya mabishano ya siku kadhaa.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa mwito huo, katika hali ambayo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuwa, namna Israel inavyoendesha operesheni yake ya kijeshi inaweka vizuizi vikubwa katika usambazaji wa misaada katika ukanda huo uliozingirwa.
Ijumaa ya jana, Desemba 22, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kuongeza misaada ya kibinadamu kwa watu wa Ukanda wa Gaza bila kutoa wito wa kusitishwa mapigano.
Pamoja na hatua hiyo kuonekana kuwa ni nzuri lakini wengi wanasema haitoshi bali kuuna haja ya kusitishwa vita huko Gaza.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imelitaja azimio hilo la Baraza la Usalama la UN kuhusu Gaza kuwa ni "hatua ambayo haitoshi" kwa ajili ya kukomesha mapigano na kushughulikia mgogoro wa kibinadamu huko Gaza.
Taarifa ya Hamas imesema kwamba, Baraza la Usalama lina wajibu wa "kuhakikisha kiasi cha kutosha cha misaada ya kibinadamu kinawasili katika maeneo yote ya Ukanda wa Gaza, hasa katika maeneo ya kaskazini." Hamas pia imesema kuwa azimio la Baraza la Usalama lilipaswa kutoa mwito wa kusitishwa mara moja operesheni za kijeshi za Israel katika Ukanda wa Gaza.