Balozi wa Yemen mjini Tehran: Tutapiga shabaha yoyote ya Marekani, Uingereza
Balozi wa Yemen nchini Iran anasema kuwa vikosi vya jeshi la nchi yake vitashambulia vituo vyote vya Marekani na Uingereza "vinavyoweza kulengwa shabaha" kujibu mashambulizi ya hivi karibuni ya nchi hizo katika ardhi ya Yemen.
Ibrahim Mohammad al-Deilami alitoa kauli hiyo katika matamshi yaliyochapishwa na Shirika la Habari la Iran (IRNA) jana Jumapili wakati akifafanua kuhusu operesheni za jeshi la majini la Yemen dhidi ya meli za Israel katika Bahari Nyekundu katika fremu ya kuwaunga mkono Wapalestina wa Ukanda wa Gaza, huku vita vya utawala huo ghasibu dhidi ya eneo hilo linayozingirwa vikiingia mwezi wa tano.
Operesheni za kijeshi za Jeshi la Yemen na harakati ya mapambano ya Ansarullah zimeisababishia Israel hasara kubwa ya kiuchumi na hivyo kuzifanya Marekani na Uingereza zianzishe mashambulizi katika mikoa ya Yemen ili kukabiliana na operesheni za nchi hiyo za kuwatetea watu wa Palestina wanaoendele kuuawa bila huruma.
“Hatua ya watu na jeshi la Yemen ni jibu la kimaumbile la kuwaunga mkono na kuwatetea watu wanaodhulumiwa na kuzuia dhulma, kwani huo ndio msimamo wa kila mtu mwenye uwajibikaji wa hali ya juu, na haifai kwa Waislamu kutojali suala hili na kutochukua hatua yoyote,” amesema Deilami.
Ameongeza kuwa: "Tunaamini kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel hauwezi kustahamili hasara zaidi, kwani hasara zake katika uwanja wa kiuchumi, kijeshi na kimaadili zimeudhoofisha utawala huo."
Balozi wa Yemen mjini Tehran amesema: "Sana'a ina wajibu wa kuendelea kutekeleza majukumu yetu ya kuwatetea watu wa Palestina hadi mwisho wa uchokozi na kuondolewa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Wapalestina."
Ibrahim Mohammad al-Deilami ameashiria misimamo ya Yemen inayosisitiza kwamba hujuma za Marekani na Uingereza hazitapita bila jibu na kusema: “Operesheni tunazozifanya kwa nguvu zetu zote dhidi ya malengo na maslahi ya Marekani na Uingereza katika Bahari Nyekundu na Bahari ya Arabia ni sehemu ya majibu haya. Sasa tuko katika vita vya pande zote na nchi hizo mbili na tutapiga kila shabaha ya adui ndani ya maeneo tunayoweza kuyalenga."