Hamas: Israel inalenga ‘kufuta uwepo wote wa Wapalestina’
(last modified Fri, 22 Nov 2024 02:33:05 GMT )
Nov 22, 2024 02:33 UTC
  • Hamas: Israel inalenga ‘kufuta uwepo wote wa Wapalestina’

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas,  inasema kuwa lengo pekee la utawala wa Kizayuni wa Israel ni "kufuta" Wapalestina kikamilifu kutoka katika ardhi za Palestina.

Khalil al-Hayya, afisa wa ngazi ya juu wa Hamas aliyasema hayo Jumatano kupitia Televisheni ya al-Aqsa ya Palestina.

Amesema utawala vamizi wa Israel unalenga kila mtu - unashambulia hospitali,  wanawake, watoto na wazee na maeneo mengine ya raia na kuongeza kuwa utawala huo unalenga "kuwatimua wakaazi wote wa Gaza, na kuwaondoa watu wa Palestina ili kutimiza ndoto zake za kuunda utawala wa Kiyahudi na Kizayuni kote Palestina."

Matamshi hayo yametolewa wakati vita vya mauaji ya halaiki vya utawala haramu wa Isarel dhidi ya Gaza vilivyoanza  Oktoba 2023 vimepelekea kupoteza maisha Wapalestina 44,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Ameishutumu Marekani kwa kupinga maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambayo yanalenga kuleta uwezekano wa kusitishwa vita hivyo, akisema hilo linaonyesha "ushirikiano wa Washington katika mauaji ya kimbari" dhidi ya Gaza.

Amemwita Waziri mkuu wa utawala haramu wa Israel Benjamin Netanyahu kuwa ni "kizuizi kikuu" katika njia ya kusitisha vita.

Hayya pia ameonya kwamba utawala wa Kizayuni unalenga kupanua vita zaidi ya Gaza, lakini akasisitiza kwamba malengo hayo ya Israel hayatafikiwa kamwe.