Netanyahu anasa kwenye dema la Mahakama ya Uhalifu
(last modified Tue, 28 Jan 2025 02:56:58 GMT )
Jan 28, 2025 02:56 UTC
  • Kkatili Benjamin Netanyahu
    Kkatili Benjamin Netanyahu

Baada ya kusita kwa muda wa mwezi mmoja, hatimaye mahakama ya kesi za uhalifu ya Israel imeanza tena kusikiliza kesi za uhalifu za waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Vyombo vya habari vimetangaza kuwa, jana Jumatatu, Benjamin Netanyahu alifika mbele ya Mahakama ya Jinai ya Tel Aviv kuwasilisha utetezi wake katika kesi za ubadhirifu na rushwa.

Kwa muda mrefu Netanyahu alikuwa anakwepa kupanda kizimbani kwa visingizio mbalimbali kama vile udhaifu wa hali yake mwilini na hata kuzusha vita na mauaji nje ya mipaka ya utawala wa Kizayuni kama ujanja na hila za kuakhirisha kusikilizwa kesi zake na familia yake, mahakamani.

Lakini hakuna kisicho na mwisho, hatimaye madai ya hali dhaifu ya kimwili yanayotolewa na Netanyahu hayana mushtiri tena na hata alipodai kuwa amefanyiwa upasuaji na hawezi kufika mahakamani, madai hayo hayakubaliwi tena na ndio maana Mahakama ya Jinai ya Tel Aviv imeamua kuitisha vikao vitatu siku za Jumanne, Jumatano na Alkhamisi badala ya kikao kimoja ili kumuondolea visingizio nduli huyo wa Ghaza.

Hadi sasa Netanyahu ameshaburuzwa mahakamani mara sita, kwa shauri ambalo limepewa jina la "Kesi ya 4000."  

Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu anajifanya haelewi chochote kuhusu kesi zinazomkabili kwenye shauri hilo lakini inaonekana ana kesi za kujibu si katika shauri hilo tu bali pia katika mashauri mengine mengi zikiwemo shutuma za kimataifa kwa jinai zake za kutisha huko Ghaza, Palestina.